Usajili wa Morrison waibua utata

Wednesday March 25 2020

Usajili wa Morrison waibua utata,mazungumzo na staa wa Yanga, Bernard Morrison , vigogo wa Simba,simba wafanya mazungumzo na morisson,Mwanasport,

 

By Waandishi wetu

UTATA wa aina yake umeibuka baada ya vigogo wa Simba kudai kwamba walishafanya mazungumzo na staa wa Yanga, Bernard Morrison na kumpa kishika uchumba.

Simba wanadai kwamba wanajua wanachokifanya na muda ukifika vitendo vitaongea kwamba wao ndio watakaokuwa na Morrison msimu ujao na si Yanga ambao awali walikuwa wamempa mkataba wa miezi sita.

Kauli za viongozi hao wanaofanya mambo yao kimyakimya ndani ya Simba zimekuja baada ya Yanga hivi karibuni kuibuka na picha zikimuonyesha mmoja wa Wakurugenzi wa GSM, Hersi Said akiwa amesimama na Morrison wakiwa wameonyesha nakala za mikataba.

Simba walidai kwamba ishu hiyo ni geresha huku wakiwataka wenzao wa Yanga kutoa picha akisaini, jambo ambalo Yanga walilifanya jana na kuwaacha Simba midomo wazi.

Picha hiyo ya jana ambayo imewaacha Simba wakiwa hawaelewi imemuonyesha Morrison akiwa ameketi kulia akisaini mkataba huo huku pia akishuhudiwa na mkurugenzi wa Sheria, Wakili Simon Peter.

Mmoja wa viongozi wenye ushawishi mkubwa ndani ya Yanga alilipa Mwanaspoti picha ya mchezaji huyo akisaini huku akisisitiza kwamba wamesikia kuna wenzao wa Simba ambao walikuwa wakimshawishi Morrison aondoke Yanga na walishampatia ‘uchakavu’.

Advertisement

Mwanaspoti limehakikishiwa na Hersi kwamba mjadala wa Morrison ulishafungwa na hawana cha kujadili kwamba staa huyo anayevaa jezi namba 33 atakuwa kwao kwa miaka miwili zaidi mara baada ya miezi sita ya awali kumalizika na akawasisitiza Simba kwamba wajiandae kumkuta kwenye FA.

“Hiyo tulishafunga zamani sana hatuna cha kujadili, kwa sasa tunaendelea na mambo mengine hakuna kitu cha kujadili hapo, unawezaje kumuachia mchezaji kama Morrison. GSM wala Yanga hatuwezi kufanya makosa ya namna hiyo,” alisema Said.

Baadhi ya viongozi wa Simba wamekuwa wakidai kwamba wameshamalizana kimyakimya na mchezaji huyo ndio maana alikuwa hajasaini Yanga kabla Jangwani kuachia picha jana.

Michezo mbalimbali imesimama kutokana na janga la Corona, lakini akili ya Yanga kwa sasa wameielekeza katika kusuka upya kikosi chao cha msimu ujao pamoja na kujiimarisha katika Kombe la FA ambalo litawapa tiketi ya kurudi kimataifa mwakani.

Advertisement