Usajili Ligi Kuu kaa la moto

Muktasari:

Ligi Kuu Tanzania Bara msimu wa 2020/21 umepangwa kuanza Septemba 6, wakati baadhi ya timu zikiwa tayari kambini kwa ajili ya maandalizi yake.

Wakati zikibaki siku 24 kabla ya dirisha la usajili kufungwa, mambo matatu yanaziweka idadi kubwa ya timu za Ligi Kuu katika wakati mgumu kipindi hiki cha kuimarisha vikosi yao.

Muda mfupi wa dirisha la usajili na hali ya kiuchumi kwa klabu mbalimbali za Ligi Kuu yanaziweka timu katika presha kubwa kipindi hiki, ambacho zinajaribu kuongeza nyota wapya kikosini.

Tofauti na misimu iliyopita, klabu zilikuwa na muda wa takribani miezi mitatu ya kuendesha zoezi la usajili, safari hii dirisha la usajili limepangwa kufanyika ndani ya siku 31 (mwezi mmoja) kama ilivyotangazwa na Bodi ya Ligi Kuu (TPLB) na Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF).

Sababu ya ufupi wa muda wa usajili wa safari hii ni kutokana na kuchelewa kumalizika kwa ligi na mashindano mengine kutokana na kusimama kwa zaidi ya miezi mitatu kutokana na virusi vya corona.

Athari za ufupi wa muda wa usajili huenda zikagharimu klabu katika namna mbili, kwanza ni kutopata muda wa kutosha kusajili wachezaji ambao wataweza kuwa na ubora wa kutimiza mahitaji ya kitimu, lakini pia kushindwa kujiridhisha juu ya uwezo na ufanisi wa wachezaji wapya wa kuingia kikosini au pia kuathiri majadiliano ya mikataba mipya kwa nyota ambao, mikataba ya sasa inaelekea ukingoni.Baadhi ya timu huenda zikalazimika kufanya usajili wa haraka haraka ili kuendana na muda wa dirisha la usajili, jambo ambalo pengine linaweza kusababisha zisipate wachezaji sahihi.

Kocha wa Namungo FC, Hitimana Thiery ni miongoni mwa walioanza kuhisi ugumu wa kupata wachezaji bora na sahihi ndani ya muda mfupi kulingana na mahitaji ya timu zao kwa ajili ya msimu ujao.

“Usajili wa wachezaji wa kigeni una changamoto zaidi kwa saba-bu kocha unatakiwa ujiridhishe zaidi, sasa kwa bahati mbaya tuna muda mfupi, hivyo umakini wa hali ya juu vinginevyo unawe-za kujikuta unapata wachezaji ambao si wale ambao unawahitaji na wenye mchango katika timu,” alisema Hitimana.

Kocha wa Boma FC inayoshiriki Ligi Daraja la Kwanza, Muhibu Kanu aliunga mkono hisia hizo za Hitimana na kudai kama timu zisipojipanga vizuri, usajili wa awamu hii unaweza usilete tija.

“Timu zina muda mfupi wa kus-ajili na makocha pia hatutapata muda wa kutosha kuunganisha timu kwa maana ya wachezaji wa zamani na wale wapya, hili jambo linaweza kuwa na athari kubwa kiufundi,” alisema Kanu.

Lakini, ukiondoa suala la ufupi wa dirisha, jambo lingine ambalo huenda likazipa ugumu klabu za soka hasa zile zinazoshiriki Ligi Kuu ni suala la kiuchumi na idadi kubwa ya klabu zinakabiliwa na hali ngumu ya kifedha.

Kutokana na kutokuwa na fun-gu kubwa la fedha za kuwawezesha kushindania wachezaji bora na wa viwango vya juu waliopo sokoni, idadi kubwa ya klabu bila shaka zitalazimika kusubiria hadi timu zenye misuli ya kiuchumi kukamilisha usajili wake ili zianze kuvuna wachezaji kwa gharama za wastani au ndogo.

Hata hivyo, Simba, Yanga na Azam FC hazionekani kama zita-kuwa wahanga wakubwa wa ath-ari hiyo kutokana na nguvu kubwa ya kiuchumi ambazo zinazo.Timu hizo kwa nyakati tofauti zimekuwa zikijinasibu kufanya usajili kabambe zikitumia nguvu ya fedha ilizonazo.

“Safari hii tutahakikisha tuna-fanya usajili wa wachezaji bora, ambao wataifanya Yanga itembee kifua mbele. Uongozi wa Yanga kwa kushirikiana na wadhamini wetu, GSM tuko makini na hatutaki yaliyotokea nyuma yajirudie,” alisema Ofisa Habari wa Yanga, Hassan Bumbuli.

Lakini, timu nyingine zimejikuta zikishindwa kufanya uamuzi wowote kuhusu usajili kutokana na kujipa muda wa kufahamu hatima ya wachezaji walionao kama wataondoka au la ili kujipanga kuziba mapengo.

Kutokana na changamoto ya kiuchumi, klabu zimepanga kutofanya usajili mkubwa katika kip-indi hiki ili ziweze kumudu bajeti zao.

Miongoni mwa timu hizo ni KMC, ambayo kupitia kwa Meneja wake, Faraji Muya imesema haitofanya usajili mkubwa.“Asilimia 70 ya wachezaji wetu wana mikataba ya kuitumikia KMC, hivyo hatutofanya usajili mkubwa, utakuwa wa wachezaji wachache tu ili kuziba mapengo ya wengine ambao tumewauza,” alisema Muya.