UCHAMBUZI: Vipigo Liverpool, Man U klabu Kariakoo zijifunze

Thursday October 8 2020

 

Mchezo wa soka kuna wakati una matokeo yanayoweza kukufurahisha kiasi cha kupagawa kwa furaha lakini pia kwa upande mwingine unaweza ukakutana na matokeo yakakuumiza muda mrefu na kubaki kama historia mbaya kwako.

Hii inatokea wakati ambao unakutana na timu ambayo iko sawa, kisha kutumia nafasi kadri ya mchezo unavyokwenda na hapo kama unakutana na wachezaji wenye kiu ya kufunga, huku timu yako ni mbovu siku hiyo unaweza kukutana na kipigo cha aibu.

Tuanzie hapa unakumbuka, Septemba 27, mwaka huu, wababe wa Ujerumani, Bayern Munich walipopokea kipigo cha mabao 4-1 kutoka kwa Hoffenheim, ambapo watu wengi walishtushwa na matokeo na ukiangalia mchezo mvua hiyo ya mabao ilianza taratibu kisha ikakolea.

Hii ndio Bayern iliyoipiga mabao manane Barcelona yaa Lionel Messi, tena siku si nyingi kwani ilikuwa ni Agosti 14 tu, lakini baadaye hawakuangaliwa usoni walipewa nne wakarudi kwao kujiuliza.

Achana na Bayern nenda pale England, bingwa wa Ligi Kuu yao, Liverpool juzi tu amedhalilishwa vibaya na Aston Villa iliyokuwa na mwendo wa kuchechemea ikinusurika kidogo kushuka daraja msimu uliopita wakipigwa mabao 7-2 na kama Villa wangekuwa vizuri zilikuwa zinakwenda mpaka 10.

Kama haitoshi siku hiyohiyo Manchester United walidhalilishwa vibaya na Tottenham Hotspurs kwa mabao 6-1 - tena wakiwa nyumbani.

Advertisement

Huu ndio mchezo wa soka na klabu zote hizo hakuna hata moja inayotaka kumfukuza kocha, ila muhimu wamerudi ndani na kujitathimini kwa kina kisha kurekebisha makosa waliyoyafanya na maisha yanaendelea.

Ukomavu huo bado haujafika huku kwetu tena bado hata haujajulikana utafika lini na klabu kongwe hapa kwetu licha ya mashabiki wao na hata viongozi kushabikia pia mpira wa huko nje lakini bado hawataki kung’amua elimu hii ya soka.

Hapa kwetu nne hizo ni nyingi unaweza ukapigwa tatu tu kisha kesho yake ukayasikia mazito ambayo yangekushangaza na ukajikuta unaona kama uko kwenye dunia ya peke yako kwa kushindwa kutofautisha matukio.

Hapa kwetu kama timu hizo zinakutana kisha ukasikia kuna moja imepoteza kwa mabao kuanzia matatu kama kocha wao au wachezaji wako salama basi ni kwa muda tu wakati wowote baadaye ataondolewa tu huu ndio utaratibu wao wa soka la dunia yao.

Tumekuwa hatutaki kukubali kwamba wakati mwingine matokeo mabaya yanakuja kma hukufanya maandalizi mazuri kucheza na mpinzani wako lakini hakuna maana kwamba kocha wako hafai wala mchezaji wako amekuhujumu.

Mechi kubwa hapa zimekuwa zikipoteza vipaji vya wachezaji wengi sana ambao hupotea kwa kashfa za kuhongwa huku mashiko ya msingi yakikosekana katika tuhuma hizo wanazoangushiwa badala ya kupoteza.

Tunaweza kujifunza kupitia matokeo haya na kwamba mpaka sasa hakuna mchezaji anayelaumiwa zaidi wamerudi na kutafuta dawa ya matatizo waliyonayo katika vikosi vyao. Ukomavu huu unaweza ukatumika katika kujifunza katka klabu zetu kwa utambua kwamna kuna wakati wanaweza kupoteza vibaya lakini haina maana kwamba timu zao mbovu kiasi cha kuanza kufukuzana kuna wakati mpira unahitajimuda kuweza kuweka mambo sawa ndani ya timu husika.

Mashabiki wanatakiwa kuacha kutengeneza taarifa mbaya kwa wachezaji - unakuta timu moja inapoteza halafu mashabiki wanaanza kuzusha taarifa ambazo si sahihi kwamba fulani tulimuona na kiongozi wa timu fulani, sasa unajiuliza kwanini hawakumwambia hapo na kusubiri mpaka wapoteze?

Taarifa mpya ni kwamba mchezo wa Yanga na Simba umesogezwa mbele unaweza kukuta taarifa hii imewafurahisha sana wachezaji na makocha, kwani ndio huwa katika wakati mgumu pale matokeo mabaya yanapokuja kuliko hata mashabiki kwa kuwa wanajua hizo ndizo mechi zinazoweza kuwapatia fedha nyingi wakishinda na kupotea wakipoteza.

 

Advertisement