Tunataka fainali ya Kili Stars, Zanzibar Cecafa

Tuesday December 3 2019

Tunataka- fainali - Kili Stars- Zanzibar- Cecafa-Kombe la Chalenji -Baraza la Vyama vya Soka -Afrika Mashariki

 

KIKOSI cha timu ya taifa ya Tanzania Bara, ‘Kilimanjaro Stars’ kilitarajiwa kuingia kambini jana kwa ajili ya kujiandaa na michuano ya Kombe la Chalenji inayoandaliwa na Baraza la Vyama vya Soka vya Afrika Mashariki na Kati (Cecafa).

Zanzibar Heroes walitangulia mapema kambini kwa ajili ya michuano hiyo itakayofanyika kuanzia Desemba 7 nchini Uganda.

Kili Stars na Zanzibar Heroes zimepangwa katika kundi moja la C pamoja na mabingwa watetezi Kenya na Djibouti.

Uwapo wa mabingwa watetezi katika kundi letu unaongeza ugumu wa kundi.

Lakini maandalizi mazuri yanaweza kuleta mafanikio kwa timu mbili hizi za taifa letu katika michuano hiyo mikongwe zaidi ya mataifa barani Afrika iliyoanzishwa mwaka 1926.

Ni kweli kwamba Kenya wamelitwaa taji hilo mara nyingi zaidi yetu, lakini historia hubadilika kila uchao.

Advertisement

Rekodi zinaonyesha Uganda ndiyo inayoongoza kwa kulibeba kombe hilo mara nyingi zaidi ikilitwaa mara 39 ikifuatiwa na Kenya (21) na kisha Tanzania Bara iliyolibeba mara nane.

Tanzania Bara imemaliza katika nafasi ya pili mara 12 na ya tatu mara 17.

Zanzibar licha ya kulitwaa kombe hilo mara moja tu mwaka 1995 walipoifunga Uganda B 1-0 katika fainali, wana historia nzuri na nchi ya Uganda zinakofanyika fainali za mwaka huu kwani taji lao hilo pekee walilibeba katika ardhi ya nchi hiyo.

Jambo jingine la kujivunia kwa Zanzibar ni kwamba wamefika fainali ya michuano hiyo mara tatu na kumaliza washindi wa tatu mara 17, hivyo si timu ngeni kimafanikio katika michuano hii.

Hata uzoefu wa kushiriki ni mkubwa. Tanzania Bara ilishiriki tangu mwaka 1945 na Zanzibar tangu mwaka 1949.

Kwa maana hiyo, timu zetu hizi mbili za taifa zina kila sababu ya kwenda kufanya makubwa huko Uganda na mojawapo kurejea na kombe la ubingwa.

Licha ya kupangwa katika kundi moja tunataka kuona timu zetu hizi mbili zinafika fainali ili kujihakikishia kombe kuja nchini.

Tunataka kuona kile kilichotokea katika fainali za Mataifa ya Afrika (Afcon) 2019 nchini Misri kinajirudia pale timu mbili za kundi letu, Algeria na Senegal, ziliposonga mbele hadi kukutana katika fainali na Algeria ya kina Riyad Mahrez kutwaa ubingwa.

Tunatambua kunakuwa na ushindani mkubwa zinapokutana timu hizi mbili za Tanzania katika michuano mbalimbali ikiwamo hii ambayo awali ilifahamika kama Gossage Cup (ilikuwa ikidhaminiwa na wazalishaji wa sabuni ya Gossage).

Lakini pamoja na ushindani, uzalendo lazima upo kwa sababu sisi ni kitu kimoja. Yeyote atakayebeba kombe hilo litakuwa ni letu sote.

Kikosi cha Zanzibar Heroes kilichojaa wachezaji mafundi kama Abdulaziz Makame ‘Abuy’, Ali Ali, Mudathir Yahaya, Feisal Salum ‘Fei Toto’, Aggrey Morris, Awesu Awesu na wengine wengi, kinabeba matumaini makubwa ya Watanzania kama ilivyo kikosi cha Kili Stars chenye nyota kibao kama Mohamed Hussein ‘Tshabalala’, Bakari Mwamnyeto, Kelvin Yondani, Ditram Nchimbi, Kelvin John ‘Mbappe’, Jonas Mkude na wengineo.

Kombe mara hii lije Tanzania.

Advertisement