Tshishimbi aomba dakika 40 tu

Muktasari:

'Nimeongea na Morisson ameahidi kuwafunga tena Simba, mashabiki wampe sapoti'

NAHODHA wa Yanga, Papy Tshishimbi hajacheza mechi hata moja tangu Ligi Kuu Bara irejee, baada ya kusimama kupisha janga la corona, lakini baada ya kujua Jumapili chama lake litavaana na Simba kwenye nusu fainali ya Kombe la Shirikisho (ASFC) ameomba apewe dakika 40 tu kuliamsha pale Taifa.

Tshishimbi amefichua kuwa anajipanga kuwasilisha ombi kwa benchi la ufundi kutaka acheze dhidi ya Simba kwa dakika 40 tu kuisaidia timu yake, lakini hapohapo akafichua mpango mzito kuhusu Bernard Morrison huku akiwapa mashabiki wao kazi moja.

Nahodha huyo aliyekuwa majeruhi kwa sasa amepona na yupo fiti kuliamsha kwenye Kariakoo Derby.

Katika mechi yao ya kwanza ya Ligi Kuu iliyopigwa Januari 4, licha ya Simba kuwa mbele kwa mabao 2-0 Jangwani walicharuka na kumaliza dakika 90 kwa sare ya 2-2 na mchezo wao wa marudiano walishinda 1-0 kwa bao la friikii ya Morrison.

“Natamani niicheze mechi hii na ASFC, nitawaomba makocha wangu, kwani najiona nipo fiti kwa sasa, lakini bado jukumu litabaki kwangu hata dakika 40 tu zinanitosha,” alisema Tshishimbi kabla ya kufunguka siri ya Morrison aliyerejeshwa kikosini.

Kuhusu Morrison ambaye wiki mbili hizi amekuwa katika vita na uongozi wa klabu yake na Tshishimbi alisema kwamba, mashabiki wa Yanga wamtarajie Morrison tofauti kabisa.

Tshishimbi alisema amezungumza na Morrison kabla na baada ya kurejea ndani ya timu hiyo, lakini kikubwa anachotaka kukifanya Mghana huyo ni kuisaidia Yanga kushinda mechi hiyo.

“Ninaongea naye sana wakati akiwa katika huo msuguano na uongozi na hata baada ya kurejea kambini,” alisema Tshishimbi.

“Aliyotofautiana na uongozi hayanihusu, kwani naamini wakikutana katika meza moja watamalizana. Kwetu kama wachezaji ametuomba radhi kwa usumbufu tulioupata wakati akiwa nje ya timu...Kila mtu ana namna yake ya kudhibiti hasira na hata kutatua changamoto,” alisema Tshishimbi na kuongeza;

“Hatukuwa na namna zaidi ya kumwelewa na kujumuika naye kazini kama kawaida na kama mwenzetu tukiwa familia moja. Tshishimbi alisema kuelekea mchezo dhidi Simba wameongea mengi na kwamba, Morrison dhamira yake ni kuhakikisha anafuta taswira mbaya iliyojengeka kuhusu taharuki yake.”

Tshishimbi alisema Morrison sio mchezaji mdogo na anajua wapi amekosea na kwamba, alimwambia kuwa mashabiki amewahuzunisha na bahati nzuri hata yeye mwenyewe analijua hilo.

“Ameniambia amerudi kufanya kazi yake kama ambavyo alikuwa akiifanya awali, anataka kucheza mechi ya Simba na kuisaidia Yanga kushinda. Anajua nini mashabiki wanataka na ameniambia anataka kuwafunga Simba ili watu wamuelewe vizuri,” alisema Tshishimbi.

Aidha, Tshishimbi aliongeza hana wasiwasi na Morrison katika kutekeleza malengo yake hayo, lakini hilo litakuwa rahisi endapo tu atakuwa fiti kimwili.

“Sijajua huu wakati alivyokuwa nje kama alikuwa anafanya mazoezi au vinginevyo kama alikuwa anafanya mazoezi nina uhakika atafanya kweli.”

Awapa kazi mashabiki

Nahodha huyo Mkongomani alisema anachowaomba mashabiki wa Yanga wala wasimpokee vibaya Morrison katika mchezo huo ambapo, mambo yaliyoyokea ni vyema wakaachiwa viongozi wa klabu yake pamoja na Morrison mwenyewe.

“Mashabiki wao wanataka ushindi hawapaswi kuwa wakali kwa Morrison watakapomuona uwanjani. Wamshangilie kama kawaida na hayo yaliyotokea wamuachie na uongozi hata sisi kama wachezaji tumeamua kuwaachia na kikubwa tunachotakiwa ni kushirikiana naye katika kufanya kazi kwa bidii na kutekeleza malengo ya timu kwa msimu huu. Tuna kazi kubwa ya kuifanya na lazima tuitimize,” alisema.

Katika hatua nyingine, wanachama na mashabiki wa Yanga mkoani Arusha, wameichungulia mechi yao hiyo na Simba na kuamua kupiga maombi ili kuhakikisha Mnyama anakufa Taifa. Katibu wa Yanga Mkoa wa Arusha, Bahati Lumato alisema lengo la kumtanguliza Mungu katika mechi hiyo ni kuhakikisha wanapata ushindi na kusonga mbele ili kuisaka tiketi ya michuano ya kimataifa msimu ujao.

“Tumepania haswa na tutawapa sapoti wachezaji wetu ili kupata ushindi hapo Jumapili, kwani michuano hii ndio nafasi pekee ya heshima ya kutupa tiketi ya kushiriki michuano ya kimataifa mwakani,” alisema Lumato ambaye amekuwa mstari wa mbele kuhamasisha wanachama Arusha.