Yanga mabingwa Kombe la Muungano 2025

Muktasari:
- Maxi Nzengeli ndiye aliyefunga bao pekee lililoipa Yanga ushindi huo dakika ya 45 akimalizia pasi ya Farid Mussa.
TIMU ya Yanga imetwaa ubingwa wa Kombe la Muungano baada ya kupata ushindi wa bao 1-0 dhidi ya JKU katika mchezo wa fainali uliochezwa leo Mei Mosi, 2025 kwenye Uwanja wa Gombani kisiwani Pemba
Maxi Nzengeli ndiye aliyefunga bao pekee lililoipa Yanga ushindi huo dakika ya 45 akimalizia pasi ya Farid Mussa.
Kwa kutwaa ubingwa huo, imeifanya Yanga kuwa kinara baada ya kulibeba mara saba ikifanya hivyo mwaka 1983, 1987, 1991, 1996, 1997, 2000 na 2025.
Wakati Yanga ikibeba ubingwa na kukabidhiwa kiasi cha shilingi milioni 50, kiungo wa timu hiyo, Mudathir Yahya ameshinda Tuzo ya Mchezaji Bora wa Mashindano huku Maxi Nzengeli akiwa mfungaji bora akifunga mabao mawili licha ya kulingana na Fred Suleiman wa JKU kwani kanuni zimembeba baada ya kufunga bao lililowapa ubingwa.
Pia Tuzo ya Kipa Bora wa Mashindano hayo imeenda kwa Ahmed Issa wa JKU, wakati JKU kwa kukamata nafasi ya pili wamekabidhiwa kiasi cha shilingi milioni 30.
Michuano hiyo ambayo ilianzishwa mwaka 1982 ikiwa maalum kwa ajili ya kusherehekea Muungano wa Tanganyika na Zanzibar, mwaka huu ilianza kuchezwa Aprili 24 ikishirikisha timu nane na kufikia tamati leo Mei 1, 2025.
Katika safari ya kubeba ubingwa, Yanga ilianza kwa ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya KVZ hatua ya robo fainali, nusu fainali ikaifunga Zimamoto penalti 3-1 baada ya dakika tisini matokeo kuwa 1-1 huku fainali ikishinda 1-0 dhidi ya JKU.
Timu zilizoshiriki mwaka huu ni KMKM, Zimamoto, JKU na KVZ kutoka Zanzibara, huku Singida Black Stars, Coastal Union, Azam na Yanga zikitokea Tanzania Bara.