Tonombe: Ubingwa? Semeni kingine

MASHABIKI wa Yanga wamekuwa wakali baada ya kukishuhudia kikosi chao kikianza Ligi Kuu Bara kwa sare ya bao 1-1 dhidi ya Tanzania Prisons, lakini pia wakichoshwa na kejeli za watani wao Simba wanaotamba kuwa, hata msimu huu watabeba tena ndoo ya ligi hiyo, hata hivyo kiungo mpya wa timu hiyo, Mukoko Tonombe amewatuliza akiwaambia wasiwe na presha.

Mukoko amewataka mashabiki hao wa Jangwani watulie, kwani kama ni ishu ya ubingwa kwa Yanga msimu huu ni jambo lisilokwepeka kwa aina ya kikosi walichonacho na alichokiona ndani ya wiki mbili tangu ajiunge na timu hiyo.

Kiungo huyo kutoka DR Congo, ameliambia Mwanaspoti baada ya kukaa na wenzake kwa wiki mbili amegendua muunganiko wao kama utakubali haraka basi ushindi utakuwa mkubwa katika mechi zao na haoni kitu kitakachowazuia wasiubebe ubingwa msimu huu.

“Watu wana wasiwasi na sare? Hapana waambieni watulie mbona hii timu ni bora! Tutakuja kushinda tena vizuri tu, nimeona tuna timu nzuri wala hakuna wasiwasi ni suala la muda tu,” alisema Mukoko aliyesajiliwa na Yanga akitokea AS Vita ya DR Congo na kuongeza:

“Timu inajengwa, ingekuwa mbaya kuanza ligi kwa kufungwa, lakini tulipata sare, binafsi naona ilicheza vizuri sana magoli yalikataa tu kuingia ile mechi lakini yatafungwa mengi tu.”

Kiungo huyo mkabaji alisema ubora tofauti wa wachezaji wapya na wenzao waliowakuta unampa imani watakuwa katika afya nzuri ya kuchukua mataji msimu huu.

Alisema hatua nzuri katika kikosi chao wamekuwa wakihimizana juu ya kuhakikisha wanashinda katika mechi zao na kwamba makosa yaliyojitokeza katika mchezo wa kwanza yatarekebishwa katika mchezo ujao.

“Uzuri katika timu naona wapo wachezaji wenye uzoefu mkubwa, wale ambao wanaonekana kupungua uzoefu nao watajifunza ndio maana ya timu ila tuna timu nzuri ya kuchukua ubingwa. “Kila mchezaji hapa anataka kuona tunashirikiana na tunashinda, hiyo ni hatua kubwa ukiwa katika kikosi cha namna hiyo, hatukushinda mchezo uliopita lakini kuanzia mechi ijayo watu wataona,” alisema Mukoko aliyechukuliwa kuziba nafasi ya aliyekuwa nahodha wa timu hiyo, Papy Kabamba Tshishimbi. Katika mechi yao na Prisons, Mukoko na Tuisila walianzia benchi kabla ya kuingia kipindi cha pili na kuichangamsha timu, huku ikipoteza nafasi nyingi za wazi.

Mukoko alisema licha ya kwamba yeye ni mgeni nchini, lakini ameiangalia ligi kwa mechi za awali na kubaini itakuwa na ushindani kwanui kuna timu zinaoonekana kuwa bora, lakini ubora wao haushindani na Yanga chini ya kocha wao, Zlatko Krmpotic ambaye ameungana nao hivi karibuni kutoka Serbia.

 

MAZOEZINI NAKO BALAA

Juzi mazoezini huko Kigambini Gezaulole kikosi hicho kilionyesha hakitaki  mchezo kutokana na jinsi walivyokuwa wanapambana kwa nguvu na kama wachezaji wangekuwa wakicheza legegele wangeweza hata kuvunjwa na wenzao kwa namna kocha Zlatko alipokuwa akiwafua.

Wakiwa katika mazoezi ya kuuchezea mpira kwa kupigiana pasi wakigawanyishwa katika makundi mawili wachezaji wote waliokuwa wanaonekaa wakiwa makini kwa kushindana kwa nguvu wakati wa kukaba lakini pia umakini wa pasi.

Katika mazoezi hayo ambayo Mwanaspoti liliyashuhudia hakukuwa na akili ya kuremba kwani kila mchezaji alikuwa akipambana kwa nguvu mithili ya watu wasiojuana na kukaribia hata kuumizana ingawa baadaye wanapeana ‘fair play’ kisha maisha yanaendelea.

Kocha Zlatko hata hivyo alikataa kuzungumza chochote baada ya mazoezi hayo, akitaka aachwe kwanza afanye kazi zake ili mashabiki waone amatokeo uwanjani.

Hata hivyo baadhi ya wachezaji wa klabu hiyo walionekana kumkubali kocha huyo na kusisitiza kama kuna watu wanawachukulia poa kwa sare dhidi ya timu ngumu kama Prisons basi wasubiri mechi yao ijayo watakapoumana na Mbeya City iliyotoka kuchezea kipigo cha mabao 4-0 mbele ya KMC mapema wiki hii Uwanja wa Uhuru.