Makocha Yanga waipa ujanja Simba fainali CAFCC

Muktasari:
- Vijana wa Fadlu Davids wanahitaji ushindi wa mabao 3-0 ili kuandika historia ya kutwaa taji hilo kwa mara ya kwanza baada ya kupoteza 2-0 mechi ya kwanza yaliyowekwa wavuni ndani ya dakika 14 za kwanza za pambano lililopigwa Jumamosi kwenye Uwanja wa Manispaa ya Berkane, Morocco.
INAWEZEKANA. Ndivyo walivyosema kwa nyakati tofauti makocha wa zamani wa Yanga, Luc Eymael na Hans van der Pluijm wakiamini Simba inaweza kupindua matokeo ya mabao 2-0 dhidi ya RS Berkane katika mechi ya pili ya fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika itakayopigwa nchini wikiendi hii.
Vijana wa Fadlu Davids wanahitaji ushindi wa mabao 3-0 ili kuandika historia ya kutwaa taji hilo kwa mara ya kwanza baada ya kupoteza 2-0 mechi ya kwanza yaliyowekwa wavuni ndani ya dakika 14 za kwanza za pambano lililopigwa Jumamosi kwenye Uwanja wa Manispaa ya Berkane, Morocco.
Wakizungumza na Mwanaspoti jana, makocha hao walisema walivyotazama mechi ya kwanza wanaamini Simba bado ina nafasi ya kubadili matokeo kama itaonyesha nidhamu ya kiuchezaji, utulivu na ubunifu eneo la ushambuliaji.
Eymael ambaye kwa sasa anaifundisha Saint Eloi Lupopo ya DR Congo, alisema ubora muda mwingine si kigezo cha kuamua matokeo. “Berkane walikuwa bora zaidi katika dakika za awali, lakini baada ya dakika 20 Simba ilirejea mchezoni. Kama wangeanza na utulivu ule tangu mwanzo stori ingekuwa tofauti. Hili bado linawezekana,” alisema Eymael.
Kocha huyo alikumbushia Simba kwenye robo fainali dhidi ya Al Masry ambapo iliibuka na ushindi wa mikwaju ya penalti baada ya kukomboa mabao 2-0 ambayo iliruhusu katika mechi ya kwanza ya Cairo, Misri.
“Hiyo mechi iwe kumbukumbu kuwa Simba wakicheza kwa nidhamu na kasi wanaweza kupindua matokeo. Kwa namna nilivyowaona wana kikosi chenye wachezaji wa aina tofauti hivyo kila kitu kipo mikononi mwao japo haitakuwa rahisi. Wanatakiwa kufanya kazi kwa bidii,” alisema Eymael.
Naye Hans Pluijm, kocha aliyeinoa Yanga kwa vipindi tofauti kisha kupita Azam na Singida Big Stars ambaye kwa sasa anaishi Ghana, alisema: “Simba wana faida ya kucheza nyumbani mbele ya mashabiki wao. Kama watamudu kupata bao la mapema moja tu basi sura ya mchezo itabadilika kabisa na presha yote itahamia kwa Berkane.”
Pluijm alisisitiza kuwa mechi hiyo siyo kwa wachezaji tu, bali pia benchi la ufundi kuwa na mbinu tofauti na zile ilizotumia pambano la kwanza kwa mechi nyingine:
“Davids anatakiwa kufanya uamuzi mgumu kama kuanza na viungo wa kushambulia zaidi. Muda wa kusubiri umekwisha,” alisema Pluijm.

PABLO ATAHADHARISHA
Kocha wa zamani wa Simba, Pablo Franco ambaye anaifundisha Al-Qadsiah ya Saudi Arabia, alisema Simba inatakiwa kucheza kwa akili na siyo nguvu pekee.
“Berkane ni timu yenye uzoefu mkubwa kwenye michuano ya CAF. Watachelewesha muda na watatumia mbinu nyingi kuvuruga kasi. Simba inapaswa kuwa na subira, lakini bado iwe na kasi kwenye uamuzi wa mwisho,” alisema Pablo aliyesisitiza Fadlu akiwa na mpango mkakati mpya wa kuibana Berkane na kutengeneza nafasi za mabao Simba itaishangaza Berkane na Afrika kwa ujumla.
Nyota wa zamani na kocha wa Simba, Jamhuri Kihwelo ‘Julio’, alisema: “Huu ni wakati wa Simba kupambana kwa roho moja. Wachezaji wanapaswa kutambua kuwa historia haijengwi kwa maneno, bali vitendo.”

MSIKIE FADLU
Kocha wa Simba, Fadlu Davids alisema kikosi kimejifunza kutokana na makosa ya mechi ya kwanza na kipo tayari kwa marudiano.
“Tumefanya tathmini ya yale tuliyokosea, hasa namna tulivyoanza mchezo taratibu. Safari hii tunaanza kwa kasi, tunamaliza kwa kasi. Tunahitaji bao la mapema kuhamasisha mashabiki wetu na kuwavuruga wapinzani,” alisema.
Davids alisema atawapa uhuru baadhi ya wachezaji kubadilika ndani ya uwanja kutegemea na hali ya mchezo, jambo ambalo linaweza kuwa silaha ya kuishangaza Berkane.
MASTAA WALA KIAPO
Nahodha wa Simba, Mohammed Hussein, alisema: “Tuna deni kwa mashabiki. Tunaamini tunaweza kupindua matokeo haya. Hii ni fursa ya kuweka majina yetu kwenye vitabu vya historia ya klabu.”
Naye Shomary Kapombe aliongeza: “Tumewahi kucheza mechi ngumu zaidi ya hii. Tutaingia kwa utulivu na mpango mmoja kushinda na kutwaa kombe.”
Naye kiungo mchezeshaji Charles Jean Ahoua alisema: “Nimecheza mechi nyingi za ushindani Afrika Magharibi, lakini hakuna presha kama hii. Tuna dhamira ya kushinda na tutapigana hadi mwisho.”
KAULI YA UONGOZI
Mtendaji Mkuu wa Simba, Zubeda Sakuru alisema maandalizi yanaendelea vizuri kama ilivyokuwa katika fainali ya kwanza ambapo kama viongozi walifanya kila ambalo lilitakiwa kufanyika ndivyo wanawajibika pia katika nusu ya pili ya fainali ambayo ipo mbele yao.
“Mashabiki waje kwa wingi kuisukuma timu. Tunahitaji uwanja uwe jiko,” alisema.
TAKWIMU ZINAONGEA
Rekodi zinaonyesha Simba ikiwa nyumbani katika michezo sita iliyopita ya Kombe la Shirikisho kwa msimu huu ikiwamo ile ya raundi ya pili dhidi ya Al Ahli Tripoli ya Libya, imeshinda yote huku ikiruhusu mabao mawili katika 3-1 na Al-Masry na ile ya 2-1 dhidi ya CS Sfaxien ya Tunisia.
Mechi nyingine ilizifunga Bravos do Maquis (1-0), CS Constantine (2-0), Al Masry (2-0) na Stellenbosch (1-0).
Katika mechi sita zilizopita za Berkane ikiwa ugenini kwenye Kombe la Shirikisho Afrika imeshinda nne ikiwamo ile ya raundi ya pili dhidi ya Dadje ya Benin iliyoifumua 2-0, kisha kuinyoa Stellenbosch 3-1, Stade Malien Bamako na ASEC Mimosas kila moja kwa bao 1-0, imetoa suluhu moja dhidi ya Desportivo Lunda-Sul na kuchapwa dhidi ya CS Constantine kwa bao 1-0 katika nusu fainali.
Hii ikiwa na maana timu hiyo katika meci hizo za ugenini imeshinda nne, kutoka sare moja na kupoteza moja, lakini ikifunga jumla ya mabao saba ya kufungwa mawili tu, huku kipa wa timu hiyo Munir Mohammed akiongoza kwa kuwa na ‘clean sheet’ nane katika mechi 13, akimzidi Moussa Camara wa Simba mwenye sita katika idadi ya mechi kama hizo za michuano hiyo ya CAF hadi sasa.