Yao afanyiwa upasuaji Tunisia

Muktasari:
- Yao alifanyiwa upasuaji wiki iliyopita wa goti la kushoto baada ya awali kupona jeraha la kifundo cha mguu na nyama za paja, lililomfanya akose mechi kadhaa za timu hiyo.
YANGA imefanya uamuzi mgumu wa kumpeleka beki wa kulia, Yao Kouassi kufanyiwa upasuaji kutokana na tatizo la muda mrefu alilonalo la goti lililomuweka nje ya uwanja.
Yao alifanyiwa upasuaji wiki iliyopita wa goti la kushoto baada ya awali kupona jeraha la kifundo cha mguu na nyama za paja, lililomfanya akose mechi kadhaa za timu hiyo.
Yao anakuwa staa wa tatu wa Yanga kutibiwa nchini humo akitanguliwa na kiungo mshambuliaji wa zamani wa timu hiyo, Yacouba Songne na kipa Abuutwalib Mshery.
Tatizo lililomsumbua Yao kitaalamu linafahamika ‘ACL reconstruction ambalo kwa sasa kuna mastaa wawili Ulaya wanajiuguza akiwamo mchezaji bora wa dunia, Rodrigo Hernandez maarufu Rodri waa Man City.
Pia ndilo lililomuweka nje mshambuliaji wa Arsenal, Mbrazili Gabriel Jesus ambapo Yao atakuwa nje kwa zaidi ya mwezi mmoja ili kujiuguza.
Akizungumzia na Mwanaspoti, Yao aliushukuru uongozi wa Yanga kumpeleka Tunisia kwa matibabu akisema upasuaji ulifanyika vizuri na atarejea siku chache zijazo. “Haikuwa rahisi, lakini nililazimika kukubali upasuaji ili nimalize hili tatizo. Namshukuru Mungu upasuaji ulikwenda vizuri, naishukuru sana klabu yangu kwa hatua hii, lakini madaktari wote,” alisema Yao.
“Nitarudi Tanzania ndani ya siku chache niendelee na matibabu. Nachoshukuru upasuaji ulikwenda vizuri.”
KUHUSU MKATABA
Yanga bado inataka kuendelea na Yao, japo mkataba alionao unamalizika mwisho wa msimu huu, lakini mabosi wanafikiria kumpa wa mwaka mmoja huku akiendelea kupona taratibu.
Yanga ina uhakika wa kuendelea kuwatumia mabeki Israel Mwenda na Kibwana Shomari, ingawa mabosi wanafikiria kusajili beki mwingine wa kulia wakitaka kumalizana na Ibrahima Keita wa TP Mazembe.
Mwanaspoti liliwahi kuripoti kuwa beki huyo ameshafanya mazungumzo na Yanga, lakini hawajafikia makubaliano, huku mkataba wake na klabu hiyo ukimalizika msimu huu.