Simba yavuna Sh 100 milioni za Ubingwa

Muktasari:

  • Kwa kipindi cha misimu mitatu mfululizo, Simba imevuna kiasi cha Sh 300 milioni kutoka SportPesa kama bonasi za kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu.

Wadhamini wa Simba, kampuni ya SportPesa leo imeizawadia timu hiyo hundi ya Shilingi 100 milioni kwa kitendo cha timu hiyo kujihakikishia taji la ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara msimu huu.
Fedha hizo ni bonasi kwa Simba kama ilivyoainishwa katika mkataba wa udhamini baina ya kampuni hiyo ya ubashiri wa matokeo ya michezo na klabu hiyo.
Hafla ya makabidhiano ya hundi hiyo imefanyika leo jijini Dar es Salaam katika makao makuu ya kampuni ya SportPesa yaliyopo Masaki.
Akizungumza katika hafla hiyo, Mkurugenzi wa Utawala na Udhibiti SportPesa, Tarimba Abbas alisema mafanikio ya timu hiyo yameipa heshima kubwa kampuni yake.
“Simba imeitendea haki nembo yetu SportPesa na na kampuni inaamini sisi kuwawadhamini wakuu imekuwa ni moja ya chachu iliyosababisha Simba Sports Club
kuchukua ubingwa huu.
“Tunachokifanya leo ni kutimiza moja ya ahadi tuliyotoa wakati tunasaini mkataba
wa udhamini mwaka 2017 kuwa tutatoa bonasi ya Sh 100 milioni endapo mojawapo ya timu tunazozidhamini itachukua ubingwa wa Ligi Kuu, hivyo bila shaka timu hiyo ni Simba," alisema Tarimba
Mtendaji Mkuu wa Simba, Senzo Mazingisa alisema kuwa utekelezaji huo ni ishara tosha ya mchango mkubwa wa kampuni hiyo kwa klabu ya Simba.
"Ushindi uko kwenye damu sisi kama wanasimba na kwa msimu huu tumeweza
kuweka historia kwa kuibuka mabingwa wa ligi kuu ikiwa bado tuna mechi sita
kuchezwa.
Moja ya jambo ambalo Simba inajivunia msimu huu ni kuwa na mdhamini kama
SportPesa ambaye mbali na udhamini, pia tumekuwa tukishirikiana katika shughuli
mbalimbali za kiuongozi," alisema Mazingisa.
Jumapili, Juni 28, Simba ilitangazwa rasmi kuwa bingwa wa Ligi Kuu msimu huu baada ya kutoka sare ya bila kufungana na Prisons ya Mbeya, matokeo yaliyowafanya wafikishe pointi 79 ambazo hazitoweza kufikiwa na timu nyingine yoyote kwenye ligi.