Simba hii Kagera atakufa tu, tena kwao

Saturday September 21 2019

 

By Doris Maliyaga

Dar es Salaam. Kagera Sugar imeipania Simba lakini Wekundu wa Msimbazi hao, wamesisitiza mchezo huo wanauchukulia umakini kama ambavyo hucheza na Yanga na wamesisitiza lazima washinde.
Simba wanasisitiza ushindi huo kwa Kagera kwa sababu iliwafunga katika mechi zote mbili za Ligi Kuu msimu uliopita yaani nyumbani na ugenini.
Wachezaji wa Simba wamesema, wana morali na mchezo huo kuona wanafanya mageuzi ya msimu uliopita.
 Mshambuliaji, Rashid Juma alisema: "Safari hii Kagera Sugar lazima wafungike kwa sababu inawezekana, safari hii hakuna kutoa pointi kwao kabisa piga ua lazima tufanye kweli."
Alisema, hata kama yeye hajapata nafasi ya kucheza, anaamini kwa sababu kila mchezaji anawaza hilo, wale watakaocheza watafanya kweli.
Beki wa kati, Yusuf Mlipili alisema: "Safari hii tutafanya kila liwezekanalo kuona tunaifunga Kagera. Hii wasitegemee mtelemko kabisa."
Mmoja wa kiongozi wa Simba ambaye hakutaka jina lake litajwe alisema; "Kwa namna ambavyo tumejipanga kuicheza mechi ya Kagera ni kama ambavyo tunajiandaa kucheza na Yanga kwa sababu jamaa wale wanatamba sana, wamekuwa wakitufunga tunakuwa hatuko vizuri wenyewe wanaona shangwe safari hii wasahau."
Simba na Kagera Sugar zinatarajiwa kucheza mechi ya Ligi Kuu Bara kwenye Uwanja wa Kaitaba, Kagera.

Advertisement