Senzo awapa ujumbe wanaYanga

Mshauri wa Klabu ya Yanga, Senzo Mazingisa amewataka wanayanga kuendelea kuwa kitu kimoja ndani ya timu hiyo ili kuhakikisha wanapata mafanikio kwa pamoja.

Senzo alitua Yanga akitokea Simba alikokuwa kama Mtendaji Mkuu wa klabu hiyo (CEO), huku kuhama kwake kwenda Yanga kukizua sintofahamu kubwa kutokana na aina ya uondokaji wake.

Katika ukurasa wake wa Instagram leo Septemba 9, 2020 Senzo ameandika ujumbe huo umelenga mipango yao ndani ya msimu huu kwa kuwagusia wachezaji, viongozi, benchi la ufundi sambamba na mashabiki.

"Tuijenge klabu yetu kwa pamoja, tujikite katika klabu yetu, kwa kuwapa kipaumbele viongozi wetu, wanachama na wafanyakazi wetu wa klabu,"ameandika Senzo.

Aidha Senzo amesema pia kwa umoja wao watazingatia kamati ya ufundi na wachezaji wa klabu hiyo kwa kuamini kwa pamoja wanaweza.

"Timu ya Wananchi Daima Mbele nyuma mwiko,"ameandika Senzo katika ukurasa wake wa Instagram hii leo.