Senzo afichua dili la Simba kumtaka Kaze

MSHAURI wa uongozi wa Yanga, Senzo Mazingisa amefichua kwamba alikuwa kwenye mpango wa kumuajiri Cedrick Kaze kuwa Kocha wa Simba kuchukua nafasi ya Patrick Aussems, lakini akazidiwa nguvu ya ushawishi.

Senzo, ambaye alikuwa Ofisa Mtendaji Mkuu wa Simba kabla ya kutema mzigo na kuibukia Yanga ameweka wazi kwamba, Kaze alikuwa ni mmoja wa makocha waliokaribia kuchukua nafasi Simba.

“Wakati tunatafuta mrithi wa Aussems (Patrick), Kaze alikuwa mmoja wa makocha walionivutia nilitamani sana angetua pale, lakini baadaye nilizidiwa nguvu na wengi, kwangu huyu alikuwa kocha bora anayeijua kazi yake,” alisema Mazingisa ambaye ni raia wa Afrika Kusini.

“Niliona aina ya falsafa yake na klabu ambayo anaifanyia kazi, sio rahisi klabu kama Barcelona kumpa mtu ajira kama yeye lakini walimuamini, nafurahi sasa niko naye hapa Yanga na ameanza kuonyesha nilikuwa sahihi wakati ule,” alisema Senzo.

Bosi huyo alisema ndani ya siku chache angalau sasa ameanza kuona ubora wa wachezaji ukirejea na kuanza kuvutia na kurudisha uhalisia wao wakiwa uwanjani.

Senzo alisema tangu ujio wa Kaze amekuwa akiifutilia timu hiyo mazoezini na sasa taratibu anaanza kuona ubora halisi wa wachezaji ukirejea baada ya anguko kubwa hapo awali.

“Naona kuna wachezaji wengi wakianza kurejea katika ubora wao hili limenivutia na kumbuka kocha ana siku chache hapa na hii timu, wengi hapa walikuwa wanapotea kwa kuanguka katika viwango vyao hili liliniumiza sana kila nilipokuwa naliona,” alisema Mazingisa.

“Unajua wadhamini na klabu walisajili wachezaji bora ambao hapa kati hawakuwa na kocha sahihi kila mchezaji uliyekuwa ukimuangalia alikuwa anacheza kwa uwezo wake binafsi, hili halikuwa zuri kabisa na ndio maana tulihakikisha tunafanya mabadiliko ya haraka,” alisema Alisema anaamini hata washambuliaji wao muda si mrefu watarudi katika ubora wao wa kufunga zaidi mara baada ya kuanza kushika kile ambacho kocha anataka wakifanye.

Alisema Yanga ina washambuliaji wazuri ambao, watakuwa na nguvu kubwa katika kufunga ndani ya siku chache zijazo endapo watashika kwa haraka mafunzo ya Kaze.

“Huyu Kaze ndio maana klabu ilielekeza nguvu kwake ni kocha, ambaye atairudishia klabu hii enzi zake za kutamba kama ilivyokuwa miaka ya nyuma,” aliongeza Senzo ambaye ni mzoefu wa soka la Afrika.

Kuanzia kesho Jumatatu Oktoba 26, 2020 tutaanza kuchapisha mfululizo wa mahojiano maalumu ambayo Senzo amefanya na Mwanaspoti. Ndani ya mahojiano hayo amefunguka mambo mazito. Usikose kufuatilia.