SHIKAMKONO : Nimefilisika kwa sababu ya Simba SC

Muktasari:

Kila mtu uwanjani hapo alikuwa anamwangalia yeye. Ni watu wachache tu ambao hawamtambui mtu yule na wanabaki na maswali yao.

BENZI rangi nyeusi linasimama pembeni mwa Uwanja wa Taifa (sasa Uwanja wa Uhuru) jijini Dar es Salaam na anashuka mwanaume mmoja mfupi na mtanashati.

Siku hii kuna mchezo wa soka kati ya Simba na timu nyingine ya Ligi Daraja la Kwanza (sasa Ligi Kuu) na watu wengi wamefurika uwanjani kuishuhudia timu yao ya Simba.

Mwanaume huyo wa enzi za miaka 80 alikuwa akitembea kwa kujiamini kuelekea wanapokaa watu mashuhuri katika mojawapo ya jukwaa la uwanja huo.

Kiunoni mwake unaonekana mkanda mweusi uliopita kwenye pindo za suruali ya kitambaa iliyochomekewa shati la maua lenye mikono mirefu. Kiatu cheusi kilichopigwa kiwi inayong’ara kukamilisha utanashati wake.

Rangi ya mwili wake inoonyesha ukwasi alionao na bila shaka hapigwi na jua. Benzi alililolipaki dakika chache zilizopita uwanjani hapo lilitoa jibu la swali hilo bila ya wasiwasi wowote. Anaonekana ni mtu mwenye kujitosheleza kwa kila kitu. Anamiliki kila anachokitaka katika maisha yake, benzi la thamani na magari mengine kadhaa, mke wa Kiarabu unadhani maisha yanataka nini tena?

Kila mtu uwanjani hapo alikuwa anamwangalia yeye. Ni watu wachache tu ambao hawamtambui mtu yule na wanabaki na maswali yao.

Anapofika karibu na jukwaa la mashabiki na wanachama wa Simba katika jukwaa la Magharibi anavua miwani yake ya jua ‘sun gogles’ na kuinua mkono wake wa kulia kuwapungia.

Mashabiki wanalipuka kwa shangwe, kumshangilia na baadhi ya watu wanalitaja jina lake kwa ufupi, Shikamkono.

Ndio ni Jabiri Ally Shikamkono. Mwanaspoti wiki iliyopita limefanya juu chini kumsaka mtu huyu na kufanya naye mahojiano ya kina.

Mwandishi wa makala haya, MOHAMMED KUYUNGA amefunga safari ya kilometa 224 kwa Reli ya Tazara hadi Kisaki mkoani Morogoro kumfuata mfadhili huyo wa zamani wa Simba ambaye inadaiwa amefilisika kutokana na kuisaidia klabu hiyo yenye maskani yake Barabara ya Msimbazi, Kariakoo jijini Dar es Salaam.

Kama kilometa hizo hazitoshi, mwandishi wetu akaongeza nyi mbili kwa bodaboda hadi Kijiji cha Gomero kumpata Shikamkono.

Jina la Shikamkono ni maarufu katika kijiji hicho hata ukimuuliza mtoto mdogo atakuelekeza kutokana na ukoo huo kumiliki nyumba kadhaa kijijini hapo.

Saa nne za usiku, mwandishi wetu anakutana ana kwa ana na Jabiri Shikamkono aliyekuwa amekaa uwani kwake kwenye nyumba yake na kusabahiana kisha kupiga stori za hapa na pale ambazo hazikuwa rasmi.

Mazungumzo hayo mara kwa mara yalikuwa yakikatishwa na simu alizokuwa akipigiwa Shikamkono.

“Hawa watu wanataka kujua kuhusu mechi ya Ligi ya Mabingwa Afrika ya Simba ya kesho (Jumamosi iliyopita dhidi ya Al Ahly iliyofanyika kule Misri ).

“Napata tabu sana kila kitu cha Simba hapa kijijini naulizwa miye. Mashabiki wengine wa Yanga wanataka kubishana na mimi… Nawakatalia kwa kuwa hawajui mambo mengi kuhusu mpira… Mimi nimekaa ndani ya Simba najua kila kitu, siwezi kubishana na shabiki wa Yanga kuhusu Kindoki (Klaus, kipa wa Yanga).

“Cha kushangaza sasa, hata watu wengine wa Dar es Salaam wananipigia kutaka kujua kuhusu mechi za Simba zitakuwaje,” anasema Shikamkono.

Asubuhi ya Jumamosi ndipo mazungumzo rasmi yalipoanza na Shikamkono anafunguka mazito kuhusu maisha ya Simba na jinsi alivyofilisika kutokana na kuihudumia klabu hiyo kama mali yake binafsi.

“Nilirudi nchini nikitokea Uarabuni mwaka 1989 nikiwa na zaidi ya Dola laki moja (100,000). Nikawa naihudumia Simba kama anavyofanya MO (Mohammed Dewji) hivi sasa.

“Nilihusika katika kufanya usajili wa wachezaji wengi, kulipa mishahara, posho, usafiri na mambo mengine mengi tu,” anasema.

Shikamkono anasema awali aliikuwa mtu wa kawaida ndani ya klabu hiyo kabla ya kujitosa rasmi mwaka 1989.

“Nilianza kuwa mwanachama wa klabu hiyo mwaka 1975 nikiwa na kadi namba 48 chini ya Mwenyekiti wa Simba wakati huo, Mikidadi Kasanda,” anasema na kumuonyesha mwandishi kadi yake ya kwanza.

Jijini Dar es Salaam, Shikamkono alikuwa akiishi Ilala, Mtaa wa Mwanza karibu na msikiti wa mtaa huo kisha akahamia Mtaa Mtwara na baadaye Ilala Bungoni kwa Mzee Kaikai ambako ilikuwa nyumba yake ya mwisho kupanga kabla ya kuhamia kwenye mjengo wake maeneo hayo ya Bungoni.

MCHONGO WA KWENDA UMANGANI

Kazi yake ya kwanza ilikuwa katika Makumbusho ya Taifa na akahamia Natex na mwisho alifanya kazi National Steel ambako anasema neema ndipo ilipoanza kumtembelea.

Mwaka 1983 alipota mchongo wa kwenda Uarabuni na kurejea nchini mwaka 1989 na kuanza rasmi kujihusisha na masuala ya Simba.

“Wakati nilipoamua kuihudumia Simba, mama yangu mzazi alinionya sana, hakutaka kabisa nishiriki mambo hayo. Na akaniambia hao ninaowasaidia hawatanithamani nikiishiwa, lakini mpira ulikuwa ndio ulevi wangu, sikumsikiliza kwa kweli.”

“Lakini baadaye niliona kweli watu wa mpira wamenitupa na mpaka sasa hawanikumbuki.”

AUZA BENZI

Katika maisha yake ndani ya Simba, Shikamkono aliuza benzi lake ambalo lilikuwa gari la kwanza jijini Dar es Salaam na Tanzania kwa jumla kuwa na vioo vya giza ‘tinted’.

Katika kufafanua hilo, anasema hakuuza benzi hilo baada ya kufilisika, bali ni kutokana na kumgharimu sana.

“Unajua sikujua kama gari lile lilikuwa linatakiwa kutumika sehemu za baridi tu. Mara mbili paipu za AC zilipasuka nikaenda kununua Nairobi (Kenya) na baadaye Lusuka (Zambia).

“Gari lilikuwa ni modeli ya Ulaya, miye nilijibebea tu sikulijua hilo. Mwaka 1999 nilikuwa nataka kurudi nyumbani (Kisaki) nikaamua kuliuza. Nakumbuka niliwauzia watu wa Esso.”

ATEMANA NA MKE WA KIARABU

Ilidaiwa baada ya kufilisika, Shikamkono aliachana na mke wake wa Kiarabu ambaye alibahatika kupata naye watoto wawili.

“Sio kweli. Huyu niliachana naye baadaye, ingawajawaje nilikuwa naye katika pilikapilika zote zilizoihusu za Simba.

Shikamkono anakumbuka watu wengi walikuwa wakifika nyumbani kwake mapema na kumsubiri nje ya geti mpaka aamke lakini leo hii wamemsahau.

“Nadhani hawanikumbuki nimefanya nini Simba, nimefanya mambo makubwa sana. Watu wameikuta Simba pale ilipo na wanaendelea nayo.

“Kingine kichoniumiza ni hawa viongozi wa sasa hawautathamini mchango wangu. Siwasemi kwa ubaya lakini si vyema kuwathamini watu ambao wenye mchango mdogo tofauti na mimi.

“Utakuta mtu anathaminiwa kwasababu eti alicheza vizuri, au kaanzisha Simba Day!” Anashangaa

Hata hivyo, Shikamkono anasema hasikitiki kupoteza pesa zake kwa ajili ya Simba, kwa kuwa ni timu anayoipenda hadi leo na wala hamlaumu mtu kwa yote yaliyotokea.

“Kosa kubwa labda kwasababu nilipata pesa nyingi wakati nikiwa bado sijakomaa kiumri. Akili zangu haikuweza kupembua mambo kwa wakati ule,” anakumbuka.

JE, NI BADO MWANACHAMA

“Unajua tangu nilipoondoka Dar es Salaam sijarudi tena rasmi. Zaidi nilipita hapo kwa siku tatu tu nilipokuwa natokea Mwanza.

“Kule Mwanza nilikuwa nafanya biashara ya kuuza vipodozi na nguo (mitumba) katika duka la ndugu yangu. Nilikaa kule kwa miaka saba. Nilipoona mambo mabaya niliamua kurudi nyumbani.

“Nilipitia Dar, klabuni kuna watu wananikumbuka kwa kile nilichokifanya walinipokea kwa furaha sana. Nimeondoka kwa heshima Simba. Kuna baadhi ya watu walifurahi waliponiona.

“Lakini niliambiwa nipige picha kwa ajili ya kupata kadi mpya lakini sijaipata kadi hadi leo hii,” anasema kwa masikitiko.

Ndio kwanza mambo yanaanza. Kesho Ijumaa Shikamkono ataeleza nini kilitokea katika mechi ya Simba na Yanga ya 1989. Simba ikitakiwa kushinda isishuke daraja na Yanga ilitaka ubingwa. Nini kilitokea? Usikose.