Redondo amvulia kofia Baraza

Muktasari:

Amesema amekuwa akipata vitu vingi kutoka kwa kocha huyo jambo ambalo limemfanya kuwa bora na kukiri kwamba mwanzoni hakuwa katika kiwango kizuri hasa raundi ya kwanza.

KIUNGO wa Biashara United, Ramadhan Chombo ‘Redondo’ ametamba kuwa ubora wake kwasasa unatokana na mbinu anazopewa na kocha wake Francis Baraza.

Redondo amesema Baraza ni moja ya makocha bora ambao kama mchezaji ukifuata maelekezo yake basi lazima uwe katika kiwango kizuri kwani ana uwezo mkubwa kwenye ufundishaji soka.

Amesema amekuwa akipata vitu vingi kutoka kwa kocha huyo jambo ambalo limemfanya kuwa bora na kukiri kwamba mwanzoni hakuwa katika kiwango kizuri hasa raundi ya kwanza.

Kiungo huyo alisema ataendelea kupambana  kuanzia mazoezini hadi kwenye mechi atakazopangwa ili kulinda kiwango chake kiwe bora zaidi ya hapo.

“Unajua kocha wetu ni mwalimu mzuri sana kama ukiwa makini kufuata maelekezo yake lazima kiwango chako kipande sio mimi pekee yangu karibia kikosi kizima kimekuwa bora kwa sasa," amesema

Amesema kipindi hiki ambacho ligi imesimama kutokana na agizo la Serikali la kuzuia mikusanyiko kwa siku 30 kutokana na uwepo wa ugonjwa wa Covid-19 unaosababishwa na virusi vya corona ulioingia nchini hivyo anajifua kivyake kwa kufuata programu ya kocha wake.