Pogba kirusi Man United

Muktasari:

Kiungo huyo mwenye umri wa miaka 27 amecheza mechi nane tu hadi sasa msimu huu katika msimu ambao amekuwa akisumbuliwa na majeraha, na Barnes anaamini vichwa vya habari vya nje ya uwanja vinavyomzunguka vinatia “sumu” hali ya hewa Old Trafford.

LIVERPOOL, ENGLAND . ISHU ya Paul Pogba inazidi kuingia katika sura mpya na tayari magwiji wa mpira wanaona staa huyo Mfaransa ni vyema apigwe bei kuliko kuwa kirusi kikosini.

Gwiji wa Liverpool, John Barnes amewashauri Manchester United wamuuze Pogba kama hana furaha klabuni hapo.

Maisha ya baadaye ya Pogba yamekuwa yakizua maswali mfululizo wakati wote wa madirisha ya uhamisho ya siku za karibuni, na kiungo huyo amehusishwa tena na klabu za Real Madrid, Juventus na Paris Saint-Germain.

Kiungo huyo mwenye umri wa miaka 27 amecheza mechi nane tu hadi sasa msimu huu katika msimu ambao amekuwa akisumbuliwa na majeraha, na Barnes anaamini vichwa vya habari vya nje ya uwanja vinavyomzunguka vinatia “sumu” hali ya hewa Old Trafford.

“Huwezi kukaa na mchezaji asiye na furaha katika klabu ya soka, hamuwezi kumfanya yeye awe ndiye muhimu kuliko klabu na mashabiki,” Barnes alisema.

“Kiufupi, jambo hilo linaishushia thamani klabu kwa kutoheshimu watu kwa kumfanya mtu asiwe na furaha. Ni ukweli unaouma kwamba unapaswa kubaki na wachezaji wenye furaha.

“Wachezaji wanapaswa kuwapa furaha makocha na mashabiki, na kama huwezi, basi (Pogba) anapaswa kuondoka. Hii drama yote pale United, ukiiangalia kutokea nje, inaonekana kama yeye ana nguvu kubwa sana klabuni kiasi cha kumfanya kila mtu amzungumzie yeye, hali ambayo ni sumu ndani ya klabu. Anapaswa kuondoka.”

Mkataba wa sasa wa Pogba unamalizika Juni mwakani, na wakati United wana haki ya kimkataba ya kumuongeza mwaka mmoja zaidi, ripoti zinaonyesha kwamba anaweza kupatikana kwa bei poa sokoni ya Pauni 55 milioni.

KUMBE ALIONYWA

Tangu atue United, Pogba ameshindwa kuonyesha ubora wake ule aliokuwa nao wakati akiwa Juventus na kumbe alishaonywa kuwa hilo lingemtokea.

Kiungo wa zamani wa Juventus, Claudio Marchisio amebainisha kuwa alimuonya Pogba akimshauri asijiunge na United mwaka 2016.

Pogba aliweka rekodi wa kuwa mchezaji ghali zaidi duniani wakati alipoondoka Turin na kutua Old Trafford kwa ada ya uhamisho ya Pauni 89 milioni, miaka minne tu tangu alipotua Juve akitokea Man United kwa fidia ndogo.

Na wakati sasa akihusishwa na mpango wa kurejea Juve, Marchisio amesema atafurahi sana Pogba akitua Turin.

“Nitafurahi sana. Nilimueleza kwamba atakosea sana kwenda Manchester na kwamba kama alitaka kubadili upepo alipaswa kwenda Hispania sio England,” Marchisio aliiambia Tuttosport.

“Kama atarudi, litakuwa jambo chanya sana, Paul atazaliwa upya katika mazingira anayoyapenda na yaliyomfanya kuwa bora.

“Na ataipa Juventus mambo makubwa kwa sababu wanamhitaji sana mtu kama yeye pale kati: yeye ni bonge la mchezaji na anazingatia sana weledi.”