Ozil kulipia upasuaji watoto 1,000 duniani

Muktasari:

Ozil amekuwa na mradi huo wa BigShoe tangu alipobeba ubingwa wa Kombe la Dunia akiwa na kikosi cha Ujerumani huko Brazil miaka mitano iliyopita.

ISTANBUL, UTURUKI.STAA wa Arsenal, Mesut Ozil atalipia huduma ya upasuaji ya matatizo mbalimbali watoto 1,000 ikiwa ni sehemu ya kusherehekea harusi yake na mrembo wa Kituruki, Amine Gulse.
Kiungo huyo mchezeshaji anayelipwa Pauni 350,000 kwa wiki huko Arsenal alitarajia kufunga pingu za maisha na Miss Uturuki wa zamani, Amine, Ijumaa.
Ozil aliwaambia wageni waalikwa kuunga mkono jitihada zake za kuhisani mradi wake unaoitwa BigShoe ili kuchangisha pesa za kulipia huduma ya upasuaji wa maradhi mbalimbali yanayowahusu watoto.
Ozil, alisema kupitia ukurasa wake wa Twitter: “Amine na mimi tutagharimia gharama za upasuaji za watoto 1000 wenye uhitaji. Itakuwa furaha kubwa sana kama watoto wa kutoka sehemu mbalimbali za dunia watafikiwa.”
Ozil amekuwa na mradi huo wa BigShoe tangu alipobeba ubingwa wa Kombe la Dunia akiwa na kikosi cha Ujerumani huko Brazil miaka mitano iliyopita.
Moyo wake wa kusaidia watu umemfanya apewe tuzo ya Laureus Sport mwaka 2014. Staa huyo wa Kijerumani pia ni balozi wa Rays of Sunshine inayojishughulisha na mambo mbalimbali ya kusaidia huduma mbalimbali za kijamii.