Oscar ajipigia debe Arsenal

Wednesday September 16 2020
oscar pic

LONDON, ENGLAND. HII inaitwa kujipigia debe. Staa wa zamani wa Chelsea, Mbrazili Oscar amesema kwamba Wabrazili wenzake, Willian na David Luiz wamekuwa wakimpigia simu na kumtaka akajiunge na Arsenal.

Wabrazili hao watatu walikuwa pamoja Stamford Bridge kabla ya kila mmoja kuchukua njia zake, huku Luiz na Willian wakikutana tena Arsenal kwa sasa na Oscar akikipiga huko Shanghai SIGP nchini China.

Hata hivyo, kiungo Oscar amekiri kwamba moyo wake kwa sasa unataka kurudi Chelsea. Oscar, ambaye alibeba mataji mawili ya Ligi Kuu England akiwa kwenye kikosi cha The Blues alichokitumikia kwa miaka mitano baada ya kutua hapo akitokea Internacional kwa ada ya Pauni 20 milioni mwaka 2012.

Baada ya kufunga mabao 38 katika mechi 203, Oscar alitimkia China kujiunga na Shanghai SIGP kwa ada ya Pauni 60 milioni. Kwenye kikosi hicho amefunga mabao 39 katika mechi 123 akiisaidia kubeba ubingwa mwaka 2018 na mwaka jana walinyakua ubingwa wa Kombe la FA China.

Oscar, ambaye ameifungia Brazil mabao 12 kwenye mechi 47, bado ana mkataba kwenye klabu hiyo ya China hadi 2024 huku akilipwa mshahara wa Pauni 400,000 kwa wiki. Lakini, Wabrazili wenzake, Luiz na Willian wanamtaka akaungane nao huko Arsenal kupiga mzigo chini ya Mhispaniola, Mikel Arteta. Hata hivyo, Oscar mpango wake ni kucheza hadi mwisho wa mkataba wake huko Mashariki ya Mbali. Timu nyingine zinazohitaji huduma yake ni Inter Milan.

Advertisement