Old Trafford palivyogeuzwa shamba la bibi

Muktasari:

Misimu sita imeshapita tangu Ferguson alipoondika Man United na wababe hao wa Old Trafford, ambapo kwa sasa pamekuwa kama shambani kwa bibi, wajukuu wanajichumia tu mazao, wamebadili makocha wanne na hakuna afadhali.

MANCHETER, ENGLAND. UNAPAJUA Theatre of Dreams? Hapo ni uwanjani Old Trafford, ambapo kwa miaka mingi Manchester United ilikuwa ikiamini hakuna kinachoshindikana inapokwenda kucheza mechi katika uwanja wake huo wa nyumbani.

Palikuwa si mahali salama kwa timu wapinzani. Ilikuwa ukipeleka timu yako kucheza Old Trafford, kuchapwa lilikuwa suala la lazima. Ilikuwa lazima upigwe tu.

Kipindi hicho timu zilikuwa zinatetemeka zamu yao ya kwenda kucheza Ole Trafford ilipofika.

Wakati huo, Man United ya Old Trafford ilikuwa balaa. Tamba huko kwako, lakini ukija uwanjani hapo, utafungwa tu. Hiyo ilikuwa kipindi kile cha Kocha Sir Alex Ferguson.

Lakini sasa The Theatre of Dreams hapatishi tena, wapinzani wamekuwa wakija na kuchukulia tu pointi. Tangu alipoondoka Sir Alex, Old Trafford zimekuja kushinda timu nyingi sana. Hata Cardiff City iliyoshuka daraja siku hizi inakwenda Old Trafford na kushinda mechi yake. Tena si kwa kubahatisha kwa maana ya kushinda 1-0, bali inashinda kwa msisitizo 2-0.

Misimu sita imeshapita tangu Ferguson alipoondika Man United na wababe hao wa Old Trafford, ambapo kwa sasa pamekuwa kama shambani kwa bibi, wajukuu wanajichumia tu mazao, wamebadili makocha wanne na hakuna afadhali.

Kwa takwimu za misimu hiyo sita, Man United ndiyo timu iliyopata pointi chache katika mechi zake za nyumbani katika orodha ya timu za Big Six. Ndani ya misimu hiyo, Man United imekuwa chini ya David Moyes, Louis van Gaal, Jose Mourinho na sasa Ole Gunnar Solskjaer.

Kwa takwimu za mechi za nyumbani katika misimu hiyo, Manchester City ndiyo inayoongoza, ambapo kwenye msimu wa 2013/14 ilibeba pointi 52 uwanjani Etihad, 2014/15 pointi 45, 2015/16 pointi 38, 2016/17 pointi 40, 2017/18 pointi 50 na 2018/19 pointi 54 na hivyo kukusanya jumal ya pointi 279 katika mechi ilizocheza nyumbani kwa misimu sita.

Arsenal inashika namba mbili, ambapo katika msimu wa 2013/14 ilivuna pointi 44 uwanjani Emirates, 2014/15 ilipata pointi 41, 2015/16 pointi 40, 2016/17 pointi 45, 2017/18 pointi 47 na 2018/19 imevuna pointi 45 zinazoifanya kuwa na jumla ya pointi 262 katika misimu hiyo sita ilivyocheza nyumbani Emirates kwenye Ligi Kuu England.

Liverpool ipo kwenye nafasi ya tatu, ikivuna pointi nyingi nyumbani katika misimu sita kwenye Ligi Kuu England, ambapo msimu wa 2013/14 ilivuna pointi 49 uwanjani Anfield, msimu wa 2014/15 pointi 35, 2015/16 pointi 32, 2016/17 pointi 41, 2017/18 pointi 43 na 2018/19 ilivuna pointi 53 na hivyo kukusanya jumla ya pointi 253.

Chelsea ipo namba nne, ambapo Stamford Bridge imevuna pointi 251 katika misimu sita ilizocheza kwenye Ligi Kuu England tangu Ferguson alipoondoka Old Trafford. Chelsea msimu wa 2013/14 ilivuna pointi 48, 2014/15 pointi 49, 2015/16 pointi 24, 2016/17 pointi 51, 2017/18 pointi 37 na 2018/19 ilivuna pointi 42 zinazoifanya kukusanya pointi 251.

Tottenham Hotspur inashika namba tano kwa kukusanya pointi nyingi katika misimu sita iliyopita katika mechi zake ilizocheza kwenye Ligi Kuu England, 2013/14 ilivuna pointi 36, 2014/15 pointi 33, 2015/16 pointi 36, 2016/17 pointi 53, 2017/18 pointi 43 na msimu wa 2018/19 ilivuna pointi 38 nyumbani na hivyo kujikusanyia pointi 239.

Man United ndio inaburuza mkia kwenye hiyo Big Six, kwa kukusanya pointi kiduchu kuliko zote katika mechi zake ilizocheza nyumbani kwenye Ligi Kuu England tangu Ferguson alipoachana nayo akiipa ubingwa wa taji hilo.

Msimu wa 2013/14 ilipata pointi 30 uwanjani Old Trafford, 2014/15 pointi 44, 2015/16 pointi 41, 2016/17 pointi 34, 2017/18 pointi 47 na msimu wa 2018/19 ilivuna pointi 36 na hivyo kujikusanyia jumla ya pointi 232, ikiwa ni tofauti kwa pointi 47 walizovuna mahasimu wao Man City kwenye mechi zao walizocheza nyumbani.

Msimu wa kwanza tu baada ya Ferguson kuondoka hapo, Man United ilivuna pointi 30 uwanjani Old Trafford, ambapo kikosi hicho kikiwa chini ya Moyes, timu kibao zilivunja rekodi ya kushinda mechi zao za kwanza kwenye uwanja huo baada ya miaka kibao.

Kipindi pekee ambacho ilipata pointi nyingi Old Trafford ni wakati ilipokuwa chini ya Mourinho msimu wa 2017/18 ambapo ilivuna pointi 47.

Hizo ndio pointi nyingi zaidi kupata Man United kwenye uwanja wake wa nyumbani tangu Ferguson alipong’atuka Old Trafford.