Obrey Chirwa amfunika Kagere

Muktasari:

Amissi Tambwe ndiye kinara wa hat trick mpaka sasa katika Ligi Kuu Bara ndani ya misimu ya kribuni kwa kufunga sita ndani ya misimu sita aliyocheza katika Ligi Kuu Bara akiwa na Simba na Yanga kwa vipindi tofauti.

MZAMBIA Obrey Chirwa ameandika rekodi usiku huu wa Julai 5 baada ya kuwa mchezaji wa kwanza kwa msimu huu kufunga hat trick mbili katika Ligi Kuu Bara, wakati akiiongoza Azam FC kuisambaratisha Singida United iliyotangulia mapema Ligi Daraja la Kwanza (FDL) kutoka Ligi Kuu.

Nyota huyo wa zamani wa Yanga na FC Platnum ya Zimbabwe, ameshafunga mabao manne mpaka sasa wakati Azam ikiongoza kwa mabao 7-0 katika pambano la upnde mmoja linalopigwa Uwanja wa Azam Complex.

Hat trick hiyo ni ya pili kwa Chirwa baada ya ile ya kwanza dhidi ya Alliance ya Mwanza walipoifumua mabao 5-0 na kumfunika mpaka Meddie Kagere wa Simba ambaye licha ya makali yake tangu atue nchini, hajawahi kufunga hat trick mbili katika msimu mmoja.

Kagere naye alifunga mabao manne walipovaana na Singida na kuwafumua mabao 8-0, lakini hajawahi kufunga mara mbili ndani ya msimu mmoja, licha ya msimu uliopita kumaliza kama kinara wa Ufungaji akiwa na mabao 23.

Pia hii ni mara ya pili kwa Chirwa ndani ya msimu mmoja kupiga hat trick, kwani alifanya hivyo mra ya kwanza msimu wa 2017-2018 alipozitungua timu za Mbeya City wakati wakiishindilia mabao 5-0 katika mechi ya Novemba 19, 2017 kisha kurudia tena dhidi Njombe Mji walioifumua 4-0 kwenye mchezo uliopigwa Feb 06, 2018.

Mabao hayo manne ya Chirwa yamemfanya kufikisha mabao 12 akilingana na Reliants Lusajo wa Namungo na kuzidi kukoleza vita ya ufungaji bora inayoongozwa na Kagere mwenye mabao 19 akifuatiwa na Yusuf Mhilu wa Kagera Sugar mwenye 13 akiwa nafsi ya pili.

Licha ya kwamba mechi haijamalizika, lakini Azam nayo imeandika rekodi ya kupata ushindi mkubwa katika mechi ya Ligi kuu tangu walipopanda msimu wa 2008. Awali rekodi yao ilikuwa ya kuifumua Villa Squad kwa mabao 6-2 na nyingine dhidi ya JKT Tanzania waliwapiga 6-1 msimu uliopita.