Nyota hawa wanawatoa jasho Simba na Yanga

Tuesday April 7 2020

Nyota hawa wanawatoa jasho Simba na Yanga,kusimama kwa Ligi Kuu , janga la ugonjwa wa corona,simba vs Yanga,mwanasport,

 

By Saddam Sadick,Mwanza

LICHA ya kusimama kwa Ligi Kuu na michezo mingine kutokana na janga la ugonjwa wa corona, lakini imeshuhudiwa hali ya ushindani kwa wachezaji ambao wameonyesha uwezo wao hadi vigogo wa soka nchini, Simba na Yanga kuwatamani.

Ligi imesimama zikiwa zimesalia raundi tisa za mechi kuhitimisha msimu wa 2019/2020, ambapo Simba ndio inaongoza kwa pointi 71 ikipewa nafasi kubwa kutetea taji lake kwa mara ya tatu mfululizo.

Wakati michuano hiyo ikiendelea, imeshuhudiwa timu zote 20 zikionyesha ushindani ili kujiweka pazuri, na vita kali imekuwa kwa baadhi ya wachezaji ambao wameonekana kung’ara na haitashangaza kuwaona kwenye uzi mwekundu na mweupe Msimbazji au wa kijani na njano pale Jangwani msimu ujao.

Mwanaspoti imeangalia uwezo wa nyota wanaokipiga Ligi Kuu na kukuletea baadhi yao waliotesa hadi sasa na kufikia hatua ya kumezewa mate na vigogo wa soka nchini, Simba na Yanga.

Yusuph Mhilu - Kagera Sugar

Straika huyu ambaye amekulia katika klabu ya Yanga kabla ya kutimkia Ndanda, amekuwa na msimu bora kwake kutokana na kazi nzuri anayoifanya pale Kagera Sugar.

Advertisement

Licha ya kutemwa Yanga chini ya aliyekuwa kocha wake, Mwinyi Zahera kwa madai ya kutomshawishi, nyota huyo amekuwa lulu kwenye kikosi cha Mecky Maxime.

Kwa msimu huu ambao unaelekea ukingoni, Mhilu amefunga jumla ya mabao 14, ambapo mabao 11 ametupia kwenye Ligi Kuu Bara na matatu amefunga kwenye Kombe la Shirikisho na kuwafanya Yanga, ambao aliwadungua pia bao moja kati ya hayo, kummezea mate upyaa.

Nyota huyo haitashangaza kumuona msimu ujao kwenye moja ya klabu kubwa nchini kutokana na kiwango alichoonesha na kuiweka timu yake nafasi nane ikiwa na pointi 41.

Reliant Lusajo - Namungo

Hakuna ubishi kwamba miongoni mwa nyota wanaotesa hadi sasa na pengine Simba na Yanga kupigana vikumbo kuwania saini yake ni Lusajo anayekipiga Namungo FC.

Namungo ambayo inashiriki Ligi Kuu kwa msimu wa kwanza, imekuwa bora kiushindani lakini moja ya wachezaji wanaoiweka juu timu hiyo ni pamoja na staa huyu.

Lusajo ambaye alivuma na timu ya Toto Africans ya jijini Mwanza, amekuwa na msimu bora zaidi akifunga mabao 13 yakiwamo mawili ya FA na kuwavutia vigogo.

Tetesi zinasema timu hizo kongwe nchini zimeonyesha nia ya kuhitaji huduma ya mchezaji huyo msomi na huenda msimu ujao akawa katika moja ya klabu hizo.

Lusajo ameiwezesha Namungo kufuzu hatua ya nusu fainali ya Kombe la Shirikisho, lakini kama haitoshi akisaidia timu yake kuwa nafasi ya nne kwa pointi 50 kwenye msimamo wa Ligi Kuu.

Abdulmajid Mangalo - Biashara United

Havumi ila yumo. Beki huyu wa kati amekuwa na faida kubwa katika kikosi cha Biashara United, huku msimu uliopita akikumbukwa zaidi kwa kazi nzuri aliyoifanya pale Uwanja wa Taifa alipoiongoza timu yake kumenyana na Yanga.

Bao lake la umbali mrefu lililomshinda kipa Ramadhan Kabwili lilimpaisha. Mangalo ni moja ya wachezaji wenye uwezo binafsi unaoibeba Biashara United kukwepa kushuka daraja.

Nahodha huyu asiye na masihara uwanjani, msimu huu pia ameendeleza moto wake chini ya Kocha Francis Baraza na kujihakikishia namba kikosini.

Kutokana na uwezo alionao ni dhahiri Simba na Yanga zinamtamani na yeye ameshaweka wazi kuwa hachagui wala habagui timu, kimsingi mwenye kufikia maelewano yuko tayari kukipiga kwao.

Bakari Mwamnyeto - Coastal Union

Nahodha huyu amekuwa na mwenendo mzuri na kuisaidia timu yake ya Coastal Union na tayari habari zinadai kuwa Simba imeshamzengea ili msimu ujao aweze kuongeza nguvu huko Msimbazi.

Mwamnyeto mbali na kuipa mafanikio Coastal, pia anakubalika kwa kazi nzuri aliyoifanya alipopewa majukumu kwenye timu ya Taifa ‘Taifa Stars’.

Usumbufu aliowapa mastraika wa timu za taifa za Sudan na Rwanda katika michezo tofauti ya kuwania kufuzu Afcon, iliwabamba wadau na mashabiki wengi wa soka nchini na kuziba pengo la mkongwe Kelvin Yondani. Kama Simba watamnasa, watakuwa wamelamba dume.

Juma Nyangi - Alliance FC

Ni msimu wake wa pili anakipiga Ligi Kuu, jamaa anaupiga mwingi licha ya kwamba msimu huu timu yake imekuwa na matokeo yasiyovutia ikipambana kutoshuka daraja.

Nyangi, chipukizi mwenye kasi na ujanja ujanja akiwa na mpira, amekuwa ni miongoni mwa wenye rekodi nzuri ikiwamo kuipandisha Alliance Ligi Kuu msimu uliopita.

Mashuti yake ya mbali na yenye macho, yamemfanya kiungo huyu kuendelea kuaminiwa kwenye kikosi hicho cha jijini Mwanza na taarifa za chini ni kuwa huenda akatimka.

Daniel Mgore - Biashara United

Kipa huyu Kinda amekuwa na kiwango bora msimu huu na kuifanya Biashara United kuwa tishio kwenye Ligi Kuu Bara.

Ikiwa ni msimu wake wa kwanza kucheza Ligi Kuu, Mgore amecheza mechi 14 bila kuruhusu wavu wake kutingishwa na kuwa miongoni mwa wachezaji wanaoweza kula shavu katika timu kubwa.

Mgore amekuwa mhimili katika timu hiyo na kuisaidia kuwa nafasi ya 10 kwa pointi 40 katika msimamo wa Ligi Kuu akiwafunika makipa wengi wazoefu.

Adam Adam - JKT Tanzania

Nyota huyu mwenye uwezo wa kucheza winga na straika amekuwa moja ya wachezaji tegemeo katika timu ya Maafande.

Ukiachana na mabao saba aliyofunga amehusika pia kupika mengine mawili na zaidi anakumbukwa kwa bao lake safi alilowatungua Simba kwa kichwa, wakati JKT Tanzania ikishinda 1-0 pale Taifa.

Staa huyu mwenye mwili wa wastani, amekuwa na katika kiwango bora cha kutosha kuzitoa udenda timu kubwa.

Advertisement