Nyota Namungo ajipa deni

Wednesday July 8 2020

 

By Clezencia Tryphone

Licha ya kupachika mabao 10 katika Ligi Kuu hadi sasa, mshambuliaji wa Namungo FC, Blaise Bigirimana amedai kuwa ameshindwa kutimiza malengo aliyojiwekea msimu huu.

Nyota huyo raia wa Burundi mwenye umri wa miaka 28, amefichua kuwa lengo lake kuu lilikuwa ni kuibuka Mfungaji Bora wa Ligi Kuu msimu huu lakini haoni kama litafanikiwa hivyo anajipanga kwa ajili ya msimu ujao.

"Malengo ndio kila kitu. Mimi nilijipangia msimu huu niwe mfungaji bora, na jitihada zangu nilifanya lakini imeshindikana kutokana na ushindani mkubwa uliopo pale timu yetu inapokutana na nyingine.

Kila mchezaji akiingia uwanjani ndani ya dakika 90 anakuwa na lengo moja. Kama ni beki, atuzuie sisi washambuliaji kufunga hivyo akifanikiwa hata sisi kufunga inakuwa shida, lakini msimu ujao Inshallah nitaweza," amesema Bigirimana.

Bigirimana amekuwa lulu katika kikosi cha Namungo FC msimu huu akitengeneza pacha tishio ya ushambuliaji sambamba na nahodha wao, Reliants Lusajo.

Wawili hao kwa pamoja wameifungia Namungo jumla ya mabao 22 kati ya 42 ambayo timu hiyo imepachika katika Ligi Kuu hadi sasa.

Advertisement

Wakati Bigirimana akiwa amepachika mabao 10, Lusajo ndiye kinara wa kufumania nyavu ndani ya kikosi cha Namungo FC akiwa amefunga jumla ya mabao 12 hadi sasa.

Advertisement