Nyomi lamduwaza Mwakinyo, akutana uso kwa uso na Mcongo

Muktasari:

Pambano hilo litatanguliwa na mengine 12, huku kiingilio kikiwa Sh 20,000, 50,000 na 100,000, kesho Agosti 13, 2020  Alhamisi mabondia wote watapima uzito na afya tayari kupanda ulingoni.

Nyomi la mashabiki waliofurika kwenye viwanja vya Las Vegas, Mabibo jijini Dar es Salaam limemduwaza bondia Hassan Mwakinyo alipokutana uso kwa uso na Tshibangu Kayembe.

Mabondia hao leo Jumatano Agosti 12, 2020 wamekutana kwa mara ya kwanza tayari kwa pambano lao la keshokutwa Ijumaa la kuwania ubingwa wa mabara wa WBF.

Mwakinyo na Kayembe raia wa DR Congo watazichapa pambano la raundi 12 la uzani wa super welter litakalopigwa kwenye ukumbi wa Mlimani City jijini hapa.

Mabondia hao wamekutana uso kwa uso kwa mara ya kwanza, tukio lililoteka hisia za mamia ya wadau wa ndondi nchini ambao walishindwa kujizuia na kumzomea Kayembe wakati akijinadi kuwa amekuja nchini kuua.

"Mwakinyo namfahamu vizuri, ana punch 'ngumi' nyepesi, hivyo asubiri kufa tu Ijumaa," alijinasibu Kayembe huku mashabiki wakimzomea na wengine wakimkebehi kuwa hawezi kumaliza raundi zote 12.

Mashabiki hao walishindwa kujizuia na kuonyesha mapenzi yao kwa Mwakinyo ambaye walianza kwa kulizingira gari aina ya Harrier lililomleta kwenye viwanja hivyo huku wakimshangilia wakiimba na kulitaja jina lake.

Baadae mashabiki wa Mabibo Sokoni walimpa bondia huyo zawadi ya matango, huku wengine wakilisukuma gari lake wakati akitoka uwanjani hapo.

"Sikutarajia mapokezi haya, hii imedhihirisha ni namna gani mashabiki wananipenda na mimi nawaahidi, sitowaangusha," alisema Mwakinyo.

Licha ya matokeo ya pambano lake la mwisho na Arney Tinampay wa Ufilipino kuwagawa mashabiki nchini juu ya kiwango chake, Mwakinyo amewatoa hofu akisisitiza kuwa maandalizi aliyofanya kumkabiri Kayembe ni tofauti na alivyofanya kwa Tinampay.

"Wakati ule muda mwingi niliutumia kuzunguka kutangaza pambano, lakini safari hii akili na kila kitu nilielekeza kwenye mazoezi, Mcongo atajuta kudandia treni kwa mbele.

Akijibu tambo za Kayembe kuwa yeye Mwakinyo ana ngumi nyepesi, bondia huyo namba moja nchini kwenye uzani wa super welter na wa 85 duniani amesema, hayo ni maneno hivyo atamthibitishia kwa vitendo Ijumaa.