Nugaz: Bila janja janja tutashinda
Muktasari:
Nugaz alisema mechi yoyote ya 'derby' inayowakutanisha watani hao inakuwa na mambo mengi yanayofanyika lakini kwa upande wao hayatakuwepo yale ya kuwagharimu basi wana kila sababu ya kuondoka kifua mbele.
UONGOZI wa Yanga kupitia Ofisa Mhamasishaji wao, Athonio Nugaz amesema mechi yao na watani zao Simba kama hakutakuwa na ujanja ujanja au makandokando ya mchezo huo basi wataondoka na ushindi na si vinginevyo.
Nugaz alisema mechi yoyote ya 'derby' inayowakutanisha watani hao inakuwa na mambo mengi yanayofanyika lakini kwa upande wao hayatakuwepo yale ya kuwagharimu basi wana kila sababu ya kuondoka kifua mbele.
"Jambo lingine ambalo linaweza kutufanya tuondoke na ushindi katika mchezo huo kama waamuzi wote sita waliopangwa watachezesha kwa kufuata sheria kutoa maamuzi ya haki basi ushindi ni wetu.
"Tunafahamu mpira una matokeo matatu kama Yanga tupo tayari kukutana na matokeo ya aina yoyote ile lakini kiu yetu kuona Mnyama anakufa hata kama hatuna nafasi ya kutwaa ubingwa wa ligi msimu huu lakini mji wote ukae kimya kama hakijatokea kitu chochote uwanja wa Taifa," alisema.
"Tunawaheshimu Simba kutokana na kikosi chao kilivyo lakini ukiangalia timu yetu inacheza soka la kuvutia na kitimu zaidi jambo ambalo linatupa imani tunaweza kuwa bora zaidi yao siku ya mechi na tukaondoka na ushindi kama malengo yetu yalivyo," alisema Nugaz.