Ni Lebron vs Big Shaq vita ya Ligi ya NBA

NANI ni nani? Achana na ishu ya jozi za viatu vyenye saini ya gwiji wa ligi ya kikapu Marekani {NBA}, Michael Jordan iliyovuka rekodi za mauzo kufikia Dola 560,000 ambazo ni kama Sh 1.3 bilioni 1.3 lakini pia sahau kuhusu toleo maalum la mkali huyo “Last Dance” lililofichua mambo mengi yaliyomhusu Michael Jordan katika msimu wake wa mwisho akiwa Chicago Bulls.

Kuna hii ya hatma ya ligi ya NBA kuhusu kurejea kuchezwa na kumalizika ama iondolewe tu msimu huu uwe umemalizika ulipoishia au ichezwe kumalizia japo kuna utata wa ianzie hatua gani kati ya kuendelea na mechi za msimu mrefu {regular} au zile timu nane kwenye msimamo wa kila ukanda zicheze mtoano?.

Kwa wafuatiliaji wa NBA, jina la Shaquille O’Neal “Big Shaq” sio geni kwao ambapo gwiji huyu wa ligi hiyo aliyewahi kutengeneza muunganiko wa aina yake na marehemu Kobe Bryant pale Los Angeles Lakers na kutwaa mataji, amekuwa na mtazamo kinzani dhidi ya nyota wa sasa kwenye timu hiyo LeBron James kuhusu ligi ifutwe au imalizike.

Big Shaq kwa upande wake akiwa kama gwiji na mchambuzi wa NBA amesisitiza hakuna haja ya kuendelea na msimu huu uliosimamishwa na ugonjwa wa corona na badala yake ufutiliwe mbali na kuendelea na mambo mengine wakati ambao LeBron amepinga vikali mtazamo huo akisema kuanzia timu yake hadi wachezaji wengi wa ligi hiyo wanataka msimu uendelee na sio kufutwa.

King James hataki kuona msimu unaisha.