Ngoma atangaza vita mpya Azam FC

Muktasari:

Tangu amesajiliwa na Azam akitokea Yanga, Ngoma bado hajaonyesha cheche zake kutokana na kusumbuliwa na majeraha na sasa amefunguka mazito.

MSHAMBULIAJI wa Azam FC, Donald Ngoma amefunguka sababu za kuwekwa benchi ni kuzidiwa mbinu na nyota wanaocheza nafasi hiyo na kuweka wazi bado anaona namba yake kikosi cha kwanza.
Ngoma hana namba kwenye kikosi cha kwanza cha Kocha, Etienne Ndayoragije ameliambia Mwanaspoti ni mapema kuhojiwa kuhusu kukosa namba kwenye michezo mitatu iliyopita na kubainisha anafasi ya kucheza kikosi cha kwanza.
Alisema amekosa kuanza katika michezo mitatu kwa sababu mwalimu ameona vitu vya tofauti kutoka kwa nyota aliowapa nafasi na anaamini muda uliobaki ambao ni kwa ajili ya maandalizi ya mchezezo wa kimataifa dhidi ya Triangle United unatosha kumuaminisha kocha wake kuwa anastahili kuanza.
“Nimeanzia benchi kwenye mchezo wa Ngao ya jamii, Feisal Kenema kombe la Shirikisho, KMC mchezo wa kwanza wa ligi  bado tuna mashindano mengi pia ligi ndio kwanza mbichi sina shaka na uwezo na naiona namba yangu kikosi cha kwanza hivyo ni suala la muda tu,” alisema na kuongeza:
“Sipo Azam FC kukaa benchi nataka kupambania timu yangu iweze kufanya vizuri katika mataji yote inayoshiriki naamini hilo linawezekana kikubwa ni kufanya kile anachokitaka mwalimu ili niweze kufikia mafanikio na kaika makubaliano ya mkataba wangu mpya ni kuona nacheza ili kuinufaisha klabu,” alisema.
Akizungumzia malengo yao katika mashindano ya kimataifa, Ngoma alisema wao kama wachezaji wamekaa pamoja na kukubaliana wanatamani kufika hatua ya makundi ya mashindano hayo ambayo ni msimu wao wa pili kushiriki.
“Tunaanzia katika uwanja wa nyumbani dhidi ya Triangle United tuna rekodi nzuri kwenye uwanja wetu hasa mashindano ya kimataifa hivyo tunaamini tutaanza vyema na kumaliza mchezo huo Chamazi kabla ya mechi ya marudiano,” alisema na kuongeza.
“Kila kitu kinawezekana kikubwa ni namna gani tumejipanga lengo likiwa ni moja kuanzia uongozi, wachezaji na hata mashabiki zetu ambao ni wachezaji wa 12 tunawaomba wajitokeze kwa wingi kutupa ushirikiano ili tuweze kufikia mafanikio,” alisema Ngoma.