NYUMA YA PAZIA: Rafiki yako Balotelli ameharibu kijijini kwake

UNAMKUMBUKA rafiki yako Mario Balotelli Barwuah? Bado yupo. Najua atakuwa ameondoka machoni mwako lakini bado yupo. Alirudi kijijini kwao kucheza klabu ya Brescia lakini na huko pia ameharibu. Balotelli bwana!

Baada ya dunia nyingine kumchoka, Balotelli akaamua kurudi kwao katika dirisha kubwa la uhamisho la majira ya joto mwaka jana. Mrudi kwao sio mtumwa. Balotelli alizaliwa Palermo katika eneo la Brescia. Jamaa wana timu ya Ligi Kuu. Ilionekana wazi kwamba sasa Balotelli angeamua kutulia nyumbani.Baada ya kudhani amenyanyasika alipotoka ilidhaniwa kwamba Balotelli angeamua kuchagua kuishia maisha ya kitulivu nyumbani. Haijakuwa hivyo. Rais wa Brescia, Massimo Cellino anataka kuachana naye haraka iwezekanavyo.

Umewahi kuifikiria Lockdown ya Balotelli ilivyokwenda? Nadhani kama ulivyoitabiri. Ilijaa ujinga mwingi. Aliamua kufanya kipindi cha Instagram live na mcheza ngono maarufu wa Italia, Rocco Siffredi. Klabu yake ilibaki imepigwa na butwaa.

Mheshimiwa Balotelli akanogewa na Lockdown. Inaonekana alikuwa anakula nyama nyingi na kulewa. Maisha yakawa matamu. Akakacha mazoezi kwa siku 10 akisingizia ana matatizo. Una matatizo gani ambayo klabu yako haiyajui?

Aliporudi klabuni alikuwa ameongezeka uzito. Rais wa klabu amechukia na sasa anataka kuachana na Balotelli ambaye mkataba wake unatarajiwa kumalizika mwaka 2022 wakati dunia ikisubiri kombe la dunia Qatar.

Nasikia anataka kwenda Brazil. Ana ofa ipo mezani ikitokea katika klabu ya Vasco da Gama. Balotelli na Brazil wapi na wapi? Huko ndio atapotea kabisa. Watamkoma. Ile nchi ya warembo ambayo inahawaribu Wabrazil wenyewe Balotelli ataiweza?

Hawa akina Ronaldinho, Ronaldo, Adriano na wengineo wangeweza kucheza zaidi na zaidi kama wangezaliwa Ulaya. Brazil imewaharibu. Kama wenyewe imewashinda, Balotelli ataiwezea wapi? Atajikita katika kujirusha na warembo kila siku katika klabu za usiku au nyumbani kwake.

Maisha ya Balotelli yamekuwa mafupi na ya ovyo. Ilitazamiwa hivyo. Kama unadhani wachezaji wa Tanzania hawajitambui basi haujakutana na Balotelli. Jose Mourinho aliwahi kudai kwamba Balotelli ni ‘Unmanageable’ yaani akimaanisha kwamba hauwezi kumuongoza. Hakukosea.

Patrick Vieira, aliyekuwa rafiki yake wa karibu wakati akicheza Inter Milan kabla ya kumfundisha Nice ya Ufaransa alichemsha kumuongoza Balotelli pale Ufaransa. Angeweza vipi kocha wa Brescia? Walishindwa akina Roberto Mancini, Brendan Rodgers na wengineo, angeweza vipi kocha wa Brescia?

Balotelli ameyaharibu maisha yake ya soka mwenyewe. Sio kwamba anajisingizia, hapana. Ndivyo alivyo. Amezaliwa akiwa mtata na daima ataendelea kuwa hivyo. Katika soka, mwisho wa safari yake umeonekana.

Balotelli hawezi kurudi tena juu. Ameshacheza Manchester City, Liverpool, Inter Milan na AC Milan. Hii ni achilia mbali na klabu mbalimbali za Ufaransa ambako alikumbana na Vieira. Hawezi kurudi tena juu. Itakuwa maajabu yaliyopitiliza.

Kitu ambacho nakukumbusha kuhusu Balotelli ni jinsi maisha ya soka yalivyo kazi ya muda mfupi. Katika miaka saba iliyopita, kutokana na utukutu wake, Balotelli amechezea klabu saba tofauti. Na katika miaka hiyo saba kumbuka kwamba namba za miaka yake zilikuwa zinaongezeka.

Tunavyoongea ni kwamba Agosti 12 mwaka huu atatimiza miaka 30. Hii ina maana kwamba anakaribia kuondoka kabisa katika soka. Amefanya mizaha mingi ambayo imemfikisha miaka 29 akiwa katika klabu ndogo kama ya Brescia. Kwa kipaji chake, miaka hiyo ilipaswa bado kumkuta akiwa katika klabu kubwa.

Lakini kitu kikubwa zaidi ni kwamba Balotelli atatuachia jina la kipumbavu nyuma yake. Ina maana tutakuwa tunamkumbuka kwa tabia zake za utata kuliko mabao yake. Ni lini Balotelli aliwahi kufunga mabao muhimu ambayo yaliibeba timu yake au timu yake ya taifa na kuipa taji.

Anaweza kuwa alikuwepo katika baadhi ya vikosi bora kama vile kikosi cha City kilichotwaa ubingwa wa England mwaka 2011, lakini atakumbukwa kwa ile pasi yake tu dhidi ya Crystal Palace akimsaidia Sergio Aguero kufunga bao la kihistoria. Zaidi ya hapo sidhani kama Balotelli amewahi kufunga mabao 22 ndani ya msimu mmoja katika klabu yoyote aliyocheza.

Balotelli atakumbukwa pia kwa ile fulana yake iliyoandikwa ‘Why Always me’ lakini sidhani kama atakumbukwa kwa chenga za maudhi, pasi za maudhi au mashuti makali. Mchezaji mzuri huwa anakumbukwa hivi, hata kama akiwa mkorofi. Wayne Rooney alikuwa mkorofi lakini tunamkumbuka kwa mabao.

Mtu anayeitwa Eric Cantona naye alikuwa tatizo. Anakumbukwa kwa kumpiga teke shabiki wa Crystal Palace, Matthew Simmons mwaka 1995, lakin anakumbukwa zaidi kwa jinsi alivyoibadlisha Manchester United kuanzia mwaka 1993.

Sijui tutamkumbuka Balotelli kwa lipi wakati huu ambao hata timu ya kijijini kwao imemshinda. Nashindwa kumlaumu kwamba labda kuna wakati alipaswa kutuliza kichwa chini na kufanya kazi yake vema. Hata hivyo asingeweza. Ndivyo alivyozaliwa. Kuna Mario Balotelli mmoja tu.