Mwesigwa aanza kujitetea mahakamani

Friday September 20 2019

 

By Fortune Francis

ALIYEKUWA  Katibu Mkuu wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Celestine Mwesigwa (49) ameieleza Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kuwa Malinzi ni miongoni mwa wafadhili wa TFF.
Wengine waliokuwa wakifadhili shirikisho hilo ni pamoja na shahidi wa tano Mohamedi Mgoi na mjumbe wa Kamati ya Utendaji, Richard Sinantwa.
Mwesigwa alidai hayo jana mbele ya Hakimu Mkazi, Maira Kasonde wakati akiongozwa na Wakili wake, Richard Rweyongeza, kujitetea.
Mwesigwa alidai hata mara ya mwisho aliyekuwa Rais wa shirikisho hilo, Jamal Malinzi aliikopesha TFF fedha zisizopungua Sh15 milioni.
Alidai akaunti za TFF zilikuwa za kutosha laakini zilikuwa hazina fedha ambapo walikuwa wakiangalia taarifa kupitia benki na kubaini hakuna fedha.
"Kupitia kwa Malinzi mkopo wa mwisho alitupa Juni 2016. Sh 15 million kwa timu ya taifa ya Serengeti Boys alitoa kulipia matangazo ya moja kwa moja" alidai Selestine.
Mwesigwa alidai mkataba wa udhamini ulikuwa michezo inapochezwa ndani ya Tanzania mechi kazima ionyeshwe moja kwa moja kwenye chaneli ambazo wananchi wanaweza kuangalia bila kulipia
Alidai walikuwa hawalipi chochote endapo Azam Pay TV ikionyesha mechi hizo lakini wananchi walipaswa kulipia hivyo, walilazimika kuonesha kupitia Television ya Taifa (TBC)
"TBC walituomba kuonesha mechi hivyo tuliomba masafa kwa Azam ili kuwapa TBC kurusha matangazo ya moja kwa moja ambao walitukubalia lakini ndani ya saa 24, TBC walituambia hawarushi matangazo bila kulipwa Sh15 milioni" alidai.
Aliendelea kudai wakati huo  wanatutaka kulipa akaunti ya TFF haikuwa na fedha tuliandaa hundi lakini hatukuweza kukabidhi TBC kwani hakukuwa na fedha.
"Tulimpigia rais na kutuambia kuwa atatupa fedha ili kuondoa aibu ya taifa amabapo tulichukua fedha hizo na kuzipeleka benki ya DTB ndipo mechi hiyo ilirushwa moja kwa moja."
Akiendekea kujitetea Mwesigwa alidai licha ya kuzisaidia timu za Taifa, Malinzi ni miongoni mwa watu wanaosaidia TFF kwenye shughuli mbalimbali.
Alidai kutokana na vyanzo vya mapato ya TFF kutoka katika mashindano,ufadhili,udhamini na kiasikidogo ada za wanachama wadau mbalimbali wa mpira wa miguu kama CUF,FIFA ambao hutoa kwa nchi wanachama baada ya kupeleka taarifa ya ukaguzi.
"FIFA huteuwa mkaguzi ndani ya Tanzania ambapo garama za ukaguzi hulipwa na TFF ambapo kampuni ya KPMG ilikuwa ndio kampuni ya ukaguzi," alisema.
"Tulikuwa tunaenda kwa viongozi wetu, Malinzi alikuwa akitupa fedha endapo tutashindwa  kumlipa mkaguzi wa hesabu wa TFF ambaye anachaguliwa na FIFA," alidai.
Mbali na Malinzi na Mwesigwa  washitakiwa wengine katika kesi hiyo ni Mhasibu wa TFF, Nsiande Mwanga na Karani Flora Rauya.
Katika kesi  hiyo ya jinai namba 213/2017 washitakiwa hao wanakabiliwa na mashitaka 20 yakiwamo ya kula njama, kughushi, kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu na utakatishaji wa fedha wa Dola za Marekani 173,335.

Advertisement