Yanga yatua Dar es Salaam, Zahera ashangaa mechi Ndanda

Monday November 4 2019

Mwanaspoti-Yanga-yatua-Dar es Salaam-Zahera-Tanzania-ashangaa-mechi-Ndanda

 

By THOBIAS SEBASTIAN

Dar es Salaam. Kocha wa Yanga, Mwinyi Zahera amesema hakuwa na taarifa ya mchezo wao wa Ligi Kuu Tanzania Bara dhidi ya Ndanda utakaochezwa Novemba 8.
Akizungumza baada ya kuwasili leo mchana kwenye Uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere, wakitokea Misri kucheza mechi ya hatua ya mtoano Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya Pyramids, kocha Zahera alisema hana taarifa ya mechi ya ligi.
Katika ratiba ya Ligi Kuu Bara inaonyesha Yanga inatakiwa kucheza Novemba 8, dhidi ya Ndanda kwenye Uwanja wa Nangwanda Sijaona Mtwara.
Zahera alisema tangu timu inatoka Misri na hata viongozi aliokuwa nao kwenye msafara walikuwa hawana taarifa ya mechi Ndanda baada ya kufika uwanja wa ndege ndio alipatiwa taarifa hiyo na kiongozi aliyekuja kuwapokea.
"Awali nilifahamu mechi na Ndanda haitakuwa siku hiyo ya Novemba 8, na mpaka tunatoka Misri sikuwaeleza wachezaji wangu jambo lolote, lakini nimefika hapa Tanzania ndio napata taarifa ya mechi hiyo, hatuna jinsi inabidi tuanze maandalizi haraka," alisema.
"Nimewapa wachezaji wangu taarifa hiyo hapa hapa kuwa kesho Jumanne asubuhi tunakiwa kuanza mazoezi ambayo yatakuwa maandalizi ya mchezo wa Ndanda ambao tutacheza ugenini," alisema.
"Baada ya kuondolewa katika mashindano ya kimataifa nguvu na akili tunaamishia katika mashindano ya ndani ili tufanya vizuri na kurudi tena katika mashindano haya mwakani," alisema Zahera.

Advertisement