Taswira ya Mlangaboy: Fraga, Makame kuamua matokeo ya Simba na Yanga

Friday January 3 2020

Mwanaspoti-Taswira ya Mlangaboy-Fraga-Makame-Simba-Yanga- kuamua matokeo-Watani wa Jadi- Mechi

 

By Andrew Kingamkono

DESEMBA 31, 2019 Meja Abdul Mingange alitoa kali ya kufungia mwaka pale aliposema aliiandaa timu yake ya Ndanda kuja kupunguza idadi ya mabao wala sio kushinda dhidi ya Simba.
Meja Mingange alitoa kauli hiyo baada ya kuishuhudia timu yake ikipokea kipigo cha mabao 2-0 kutoka kwa vinara wa Ligi Kuu Simba kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.
Mingange alisema “Mlitaka nifunguke ili nifungwe saba?  Tulikuja hapa kwa lengo la kupunguza idadi ya mabao wala siyo kushinda.”
Nimeipenda kauli hii ya Meja Mingange ni ishara nzuri ya kuwaheshimu wapinzani wako hasa unapogundua ni bora kuliko timu yako. Nadhani makocha wengine wanapaswa kuwa wawazi na wakweli  kama Meja kwani inasaidia kuijenga timu pamoja na kuwaeleza ukweli mashabiki wako.
Ukiachana na hayo ya Mingange na Ndanda yake kesho Jumamosi Januari 4, 2020 ndiyo ile siku inayosubiriwa na mashabiki wa soka wengi nchini kuona nani atauanza mwaka kibabe kati ya Simba na Yanga.
Ni mechi inayovuta hisia kila kona ya nchi kwa mashabiki wa timu hizi kutambiana kabla na baada ya mchezo. Mechi  hii wakati mwingine inagharimu hadi maisha ya watu wengine kuzimia, kupoteza mali na mengine mengi tu, ili mradi tafrani kila sehemu.
Najua baada ya mechi hii kuna wachezaji watakuwa mashujaa, lakini wengine watakuwa wamepooza baada ya kupoteza maisha ya soka ndani ya klabu hizi.
Hata hivyo, Taswira inauangalia mchezo huu katika eneo kiungo ambalo ndilo litakaloamua mechi hii iwe na mabao mengi, machache au suluhu.
Kama wewe shabiki utapata nafasi ya kesho kwenda uwanjani kuangalia mechi hii achana na kusubiri goli alilofunga Meddie Kagere, Deo Kanda wa Simba au David Moringa au Tariq Seif wa Yanga utashindwa kufurahia mpira huo.        Tupa jicho lako katikati ya uwanja uangalie viungo.  Najua Simba wataingia fomesheni ya 4-5-1 wakijaza viungo watano katikati Mbrazili Fraga, Muzamiru Yassin, Clatous Chama, Deo Kanda, Francis Kahata au Mehboub Shiboub lengo ni kutawala mchezo kwa pasi fupifupi za uhakika kwani hiyo ni moja ya silaha kubwa ya mabingwa hao.
Nimempa nafasi Mbrazili, Fraga kuanza kutokana na uwezo wake mkubwa wa kuzuia mashambulizi ya timu pinzani na kutimiza vizuri majukumu yake ya kuwalinda mabeki, ukilinganisha na Mkude ambaye atapenda zaidi kuwafurahisha mashabiki wake wa jukwaani.
Muzamiru atakuwa na jukumu moja kubwa la kuhakikisha anaanzisha mashambulizi kwa pasi za pembeni akiwaunganisha Chama au Shiboub pamoja Kanda au Kahata hasa katika mapungufu ya kushindwa kwao kurudi nyuma kukaba.
Kocha Sven amekuwa akifanya mabadiliko makubwa ya kikosi chake kila kukicha, akitaka kuona uwezo wa wachezaji wake, lakini naamini mechi hii inaweza kuwa kipimo chake cha uvumilivu kutoka kwa wale wanaotaka kumsaidia kupanga kikosi.
Ili Yanga iweze kuimudu Simba katika mchezo huo inapaswa nayo kuingia uwanjani na fomesheni ya 4-5-1 japokuwe wenyewe ni waumini wa 4-4-2 hakuna shida kwa mfumo wowote watakaotumia jambo la msingi ni kuwa na watu sahihi.
Naamini katika kiungo wakiwachezesha Abdullaziz Makame, Fiesal Salum ‘Fei Toto’, Deus Kaseke au Mohamed Banka akiwa katika ubora wake, nahodha Papy Tshishimbi na Patrick Sibomana, hii itawafanya kuwa wengi katikati, hivyo itawanyima nafasi Simba kujipanga kutokea eneo la kati. Kiungo mwingine, Haruna Niyonzima hajawahi kuwa na msaada kwa mechi za watani wa jadi, lakini uzoefu wake unaweza kumpa nafasi kwenye kikosi cha Yanga.
 Makame ni kiungo aliyetimia anaweza kucheza mipira ya juu pasi za uhakika amekuwa siri kubwa ya ubora wa safu ya ulinzi kutokana na uwezo wake wa kukata umeme.
Fei Toto atakuwa na kazi ya kuanzisha mashambulizi ya pasi ndefu kwa Molinga au Tariq wakati Yanga itakapokuwa inafanya mashambulizi ya kushtukiza. Tshishimbi na Kaseke au Banka watakuwa na kazi kubwa ya kupika pasi za mwisho pamoja na kusaidia majukumu ya ulinzi katika eneo la kiungo. Yanga kwa asili ni timu inayofanya mashambulizi yake kupitia pembeni, hivyo Sibomana atakuwa na jukumu la kuanzisha mashambulizi kutokea huko japokuwa naye si mzuri sana kwenye ulinzi ila kasi yake inahitaji.
Tahadhari yangu kwa Kocha  Charles Boniface Mkwasa ni lazima awape heshima Simba, lakini asikubali kuanza kwa pamoja na Mrisho Ngassa na Sibomana katika mchezo huo.
Ngassa na Sibomana wote hawezi kurudi nyuma kukaba hivyo atawaongezea mzigo viungo wake pamoja na mabeki na matokeo yake atayapata.
Pamoja na yote Taswira kama wewe shabiki wa Simba mtazame Fraga au kama  Yanga, basi mtazame Makame ni wachezaji wawili wasiokuwa na vitu vingi, lakini wanajua kutimiza vema majukumu yao wanapokuwa uwanjani.
Ni viungo wakabaji waliobora zaidi katika msimu huu hakuna ubishi makosa ya Fraga au Makame kwa sehemu kubwa ndiyo yatakayoleta matokeo ya kilio au kicheko uwanjani.

Advertisement