Hisia Zangu: Fei Toto wa juzi, jana na leo anashangaza

Tuesday January 14 2020

Mwanaspoti-Tanzania-Hisia Zangu-Edo Kumwembe-Fei Toto- Yanga-Michezo blog-Mwanasport-MICHEZO-

 

By Edo Kumwembe

MCHEZAJI anayeitwa Feisal Salum ‘Fey Toto’ nimemkumbuka sana. Hakucheza mechi dhidi ya Simba na hakuna shabiki wa Yanga aliyeumia. Hakuna shabiki wa Yanga aliyehoji kwanini Fey hakucheza. Hivi ndivyo ambavyo nyakati zinavyokwenda kasi.
Majuzi timu ya taifa ilisafiri kwenda Tunisia kwa ajili ya pambano dhidi ya Libya. Fey Toto hakuwepo na hakuna shabiki aliyehoji. Hakuna aliyejali. Timu ilifungwa mabao 2-1 na kwa jinsi Watanzania ninavyowafahamu, kama Fey angekuwa wa miezi 24 iliyopita kuna watu wangehoji ‘kwanini Fey hakuitwa?’
Leo hakuna mtu anayehoji. Kama Yanga wenyewe hakuwahoji Fey kutocheza mechi dhidi ya Simba, kwanini wajali Fey kutoitwa Taifa Stars? Akiendelea hivi basi mwishoni mwa msimu atatolewa kwa mkopo kwenda KMC. Baadaye atachukuliwa jumla. Baada ya misimu miwili atakwenda Kagera Sugar. Baada ya hapo atarudi JKT Ruvu. Baada ya hapo simulizi yake itakuwa imeisha.
Huyu ndiye mchezaji ambaye Emmanuel Amunike aliwahi kuapia kwamba angeweza kucheza Barcelona. Sikuwahi kumpinga Amunike na wala sitampinga katika nyakati hizi. Sio kwamba Fey alikuwa amefikia hadhi ya kucheza Barcelona, hapana, alikuwa na kipaji ambacho kama kingesuguliwa vema tangu akiwa mtoto pale Zanzibar basi angeweza kufika Barcelona.
Kitu hiki cha kuwa na kipaji wazungu wanaita ‘potential’. Unaweza kuwa na potential lakini ikishia njiani. Leo Fey anaelekea kufikia njiani. Unajua kwanini wachezaji wa aina ya Fey wanapotea? Kuna sababu nyingi.
Kwanza kabisa klabu zetu hazina mfumo wa kumuendeleza mchezaji aendelee kuanzia pale walipomnasa. Klabu haimsaidii mchezaji. Kuanzia viongozi hadi benchi la ufundi. Klabu haijui kinachomkabili mchezaji nje ya uwanja. Mara nyingi wanamtazama mchezaji ndani ya uwanja.
Pili, mchezaji mwenyewe anaishi katika mzunguko wa kawaida wa kila siku wa maisha. Mchezaji anajiona ana mkataba na klabu. Hana presha. Anaamka asubuhi, anaenda mazoezini, anarudi nyumbani, anashinda katika duka la mangi akipiga stori, jioni anarudi tena mazoezini, akitoka mazoezini anaenda kulalala.
Sitaki kumuingiza katika dhambi za maneno ya mitaani ambayo wakati mwingine wachezaji wetu wanasingiziwa kwamba wanaharibiwa na wanawake wenye umri mkubwa, pombe na mengineyo. Fey naamini ni Muislamu safi. Lakini bado ratiba ya kawaida tu ya timu inaweza kummaliza mchezaji kama hana njaa binafsi ya kufika mbali.
Hata hizi kambi huwa hazisaidii kama mchezaji hana njaa. Akiwa kambini ratiba yake inakuwa ile ile. Mchezaji anakesha kupitia kurasa za Instagram za Diamond Platinumz, Wema Sepetu, Zari, Ali Kiba, Lionel Messi na wengineo. Analala saa tisa usiku, asubuhi anaenda mazoezini, anarudi kulala, jioni anaenda tena mazoezini.
Mchezaji haumii kutopangwa, mchezaji hatumii muda wake kujitathamini (self-assessment), mchezaji hana muda wa kujihangaisha kujiondoa nje ya ratiba ya timu. Anafurahi tu kuwa mchezaji wa Yanga au Simba.
Simba ilipopata mabao yake katika mechi ya Yanga nilimshangaa mchezaji mmoja mwenye kipaji aliyekuwa benchi akifurahi kupita kiasi. Wala hakujali kwamba alipaswa kuwa uwanjani kuonyesha mambo mkubwa katika mechi kama ile.
Nadhani Fey ameingia katika mtego huu. Sidhani kama ana hasira sana ya kutopangwa. Sidhani kama ana hasira sana ya kuondoka katika njia ya kawaida ya maisha ya kila siku. Kwa ninavyowafahamu wachezaji wa Kitanzania, mchezaji kama Fey akijiondoa tu katika ratiba ya timu akajiwekea ratiba yake binafsi basi anakuwa bora maradufu.
Nimewaona wachezaji wengi wakipotea kama Fey. Kipaji unakiona lakini juhudi zilizopitiliza hauzioni. Wanaridhika na njia ya kawaida ya maisha. Mchezaji kama Fey akiamua kuwa na hasira na kujikita katika soka kwa asilimia mia sioni kiungo wa kumfananisha naye.
Fey ndiye ambaye amemrudisha Haruna Niyonzima Yanga. Yeye na mwenzake, Abdulaziz Makame walikuwa na fursa nzuri ya kuwasahaulisha Wanayanga mchezaji anayeitwa Haruna Niyonzima. Wangekuwa wakicheza asilimia mia ya uwezo wao, hakuna ambaye angemkumbuka Haruna.
Wachezaji wetu wana homa za kupanda na kushuka. Leo ukimuona unahisi ana uwezo kama wa Kevin de Bruyne, kesho ukienda kumuona unahisi haujawahi kumuona mchezaji mbovu kama yeye. Yote haya yanatokana na ukosefu wa malengo.
Mchezaji kama Fey angekuwa ameweka malengo ya kufika kule ambako Mbwana Samatta na Simon Msuva wamefika, leo angekuwa mbali. Angekuwa na bidii mara tatu zaidi ya alivyo. Kipaji anacho kikubwa. Kama unamuona ni mchezaji wa kawaida basi ni kwa sababu anaishi katika ratiba ya timu tu.
Bahati mbaya pia kwa timu kama Yanga, ni rahisi kwa sasa kwa Fey kupotea.
Anayachukua matatizo ya timu na kuyajali.
Wachezaji wenye malengo huwa hawajali sana matatizo ya timu za dunia ya tatu. Mchezaji aliyefika anaweza kujali sana, lakini mchezaji kama Fey hapaswi kujali. Kipaji chake sio cha nchi hii.

Advertisement