Mechi mbili kuamua ubingwa wa Tanzania tenisi Afrika

Monday January 13 2020

Mwanaspoti-Mechi-Mwanasport-Tanzania-tenisi-Afrika-Michezo-MICHEZO blog

 

By Imani Makongoro

Dar es Salaam.Tanzania inahitaji ushindi katika michezo miwili ili kujihakikishia ubingwa au kuingia tatu bora katika mashindano ya Tenisi Afrika Mashariki na Kati yatakayofungwa kesho kwenye viwanja vya klabu ya Gymkhana, Dar es Salaam.

Timu ya wavulana chini ya miaka 16 inahitaji ushindi mbele ya Rwanda inayoongoza msimamo na ushindi mwingine dhidi ya Shelisheli ili kujihakikishia ubingwa huku ikiombea Burundi ambayo ni ya pili katika msimamo ifungwe na Uganda na Rwanda katika mechi za leo na kesho.

Katika kundi hilo Rwanda inaongoza ikiwa na pointi 3 baada ya kushinda michezo yake tisa, ikifuatiwa na Burundi yenye pointi tatu ingawa imeshinda michezo minane na kufungwa mmoja na Tanzania ni ya tatu ikiwa na pointi mbili, ikifungwa mechi tano na kushinda nne.

Endapo Tanzania itamfunga Rwanda baadae jioni na kesho dhidi ya Burundi itafikisha pointi tano, huku ikiombea wapinzani wake, Burundi na Rwanda wafungwe mechi zao mbili zilizosalia au hata moja moja, matokeo yatakayoipa nafasi kutwaa ubingwa msimu huu.

Nyota wa Tanzania, Kanuti Alagwa amesema wanafahamu ugumu wa mechi hizo na umuhimu wa kutwaa ubingwa wa mashindano hayo.

Kanuti katika mashindano ya mkondo wa kwanza alitwaa medali ya dhahabu amesema wako tayari kupambana ili kubakisha ubingwa nyumbani licha ya kukiri ushindani kuwa mkubwa msimu huu kulinganisha na msimu uliopita.

Advertisement

Katika mechi za mapema Asubuhi leo za vijana chini ya miaka 14, Mtanzania, Nasha Singo alishindwa kutamba mbele ya Rona Tuyishime wa Rwanda.

Nasha alikubali kipigo cha seti 2-0 za 6-1 na 6-1 katika nusu fainali ya kwanza ambayo Rona alifuzu kucheza fainali na Faith Urassa wa Kenya.

Faith alimfunga Paula Awino wa Uganda kwa seti 2-0 za 6-2 na 6-1.

Kwa wasichana chini ya miaka 16, Kenya na Uganda zitacheza kusaka bingwa kesho wakati Tanzania ikitwaa medali ya shaba.

 

 

 

Advertisement