Mbao kutembelea nyayo za Mtibwa Sugar kuimaliza Simba SC

Wednesday January 15 2020

Mwanaspoti-Mbao-kutembelea-Mtibwa Sugar-Simba SC-Michezo-Mwanasport-Michezo Blog-BBC Michezo

 

By Saddam Sadick

Mwanza.Wakati Mbao ikitarajia kushuka uwanjani kesho kuwakaribisha Simba katika mchezo wa Ligi Kuu, Kocha wa timu hiyo Abulmutiki Khaji amesema watapitia njia walizotumia Mtibwa Sugar kuwamaliza wapinzani.

Mbao iliyopo nafasi ya 14 kwa pointi 18 baada ya mechi 16, inawakaribisha Simba wanaoongoza Ligi kwa alama 35 kwa michezo 14, mchezo utakaopigwa kwenye Uwanja wa CCM Kirumba Jijini Mwanza.

Hata hivyo Simba inawakabili ‘Wabishi’ hao ikiwa na rekodi mbaya kwani mara ya mwisho kukutana timu hizo kwenye uwanja huo, walilala bao 1-0, ikiwa chini ya Kocha Patrick Aussems aliyerushiwa chupa za maji na mashabiki baada ya mpambano.

Akizungumza baada ya mazoezi asubuhi ya leo Jumatano kwenye uwanja wa Nyamagana, Khaji amesema watakuwa makini kupambana kusaka ushindi na kwamba Mtibwa Sugar tayari imewaonyesha njia.

Amesema licha ya kumkosa Nahodha wake, Said Khamis, lakini vijana wengine wako vizuri na watapambana kuhakikisha wanaibuka na pointi tatu ili kujiweka pazuri kwenye msimamo wa Ligi.

“Ukiangalia Simba ni wazuri maeneo yote, kwahiyo tumewaandaa vizuri wachezaji na hatutawapa nafasi ya kumiliki mpira, tayari Mtibwa Sugar wameshatuonyesha kwamba inawezekana” ametamba Khaji.

Advertisement

Wakati huohuo, Simba tayari wameshawasili jijini hapa tangu usiku wa kuamkia leo na saa 10 jioni wanatarajia kufanya mazoezi kwa ajili ya mchezo huo.

Advertisement