Kenya yaichapa Uganda yaikwepa Kilimanjaro Queens nusu fainali Chalenji

Thursday November 21 2019

Mwanaspoti-Kenya-yaichapa-Uganda-yaikwepa-Kilimanjaro-Queens-nusu-fainali

 

By Doris Maliyaga

Dar es Salaam.Timu ya soka ya Taifa ya Wanawake ya Kenya imeinyuka Uganda mabao 3-0 na kuikwepa Tanzania Bara katika nusu fainali ya mashindano Chalenji Cecafa wanawake yanayoendelea Uwanja wa Azam Complex, Dar es Salaam.

Tanzania Bara 'Kilimanjaro Queens' itacheza na Uganda mechi ya nusu fainali Jumamosi hii wakati Kenya itaivaa Burundi.

Katika mchezo huo Kenya waliocheza soka la kuvutia na pasi nyingi tofauti na wapinzani wao Uganda waliotumia zaidi nguvu.

Kenya ilifanikiwa kupata bao kwanza katika dakika 9, lililofungwa na Merci Airo kabla ya Mwanalima Jereko kuongeza la pili dakika ya 18 na Jentrix Shikangwa akimaliza la tatu kwa njia ya mkwaju wa penalti.

Mwanalima ambaye ni mshambuliaji na nahodha wa kikosi hicho, amekuwa chachu ya ushindi ya Kenya.

Aliwachezesha, Cynthia Musungu na Merci, pia pamoja na kucheza nafasi ya ushambuliaji alirudi nyuma kutafuta mipira.

Advertisement

Kenya na Uganda zinatoka Kundi B, zote zimeingia nusu fainali na kuziacha Ethiopia na Djibouti zikiaga mashindano hayo.

Mashindano hayo ya Cecafa wanawake yameshirikisha timu za mataifa nane kutoka Afrika Mashariki na Kati wenyeji Tanzania Bara, Kenya, Uganda na Burundi, timu nyingine zilizoshiriki ni pamoja na Djibouti, Ethiopia, Zanzibar na Sudan Kusini.

Advertisement