Hisia Zangu: Haifai Kelvin John wetu kuitwa Mbappe

Wednesday December 11 2019

Mwanaspoti-Hisia-Zangu-Tanzania-Haifai-Kelvin John-wetu-kuitwa-Mbappe

 

By Edo Kumwembe

STAA anaiyeitwa Kylian Mbappe alizaliwa siku tano kabla ya sikukuu ya Krismasi mwaka 1998. Alizaliwa Desemba 20, 1998 nchini Ufaransa, wazazi wake wakiwa wana asili ya Cameroon. Hapana shaka walizamia Ufaransa.
Staa wa Kitanzania anayeitwa Kelvin John alizaliwa Juni 10, 2003 pale Morogoro - Tanzania. Huyu Kelvin John wetu huwa anaitwa Mbappe na wachezaji wenzake wa timu ya vijana, waandishi wa habari na mashabiki wa soka.
Anaitwa Mbappe kwa kufananishwa na Kylian Mbappe. Wakati Mbappe halisi ana miaka 20, Kelvin John ana miaka 16. Wamepishana miaka minne tu. Kila ninapomtazama Kelvin John nahisi atafika mbali. Na atafika mbali muda si mrefu kuanzia sasa.
Kelvin John ana kasi, ana jicho la lango, ana akili ya mpira. Zaidi ya kila kitu kwa sasa yupo katika mikono salama ya watu wa klabu ya Genk ingawa amepelekwa England kwa uangalizi zaidi. Yupo katika njia sahihi ya soka akiwa na umri mdogo.
Ndani ya miaka miwili ijayo itakuwa ruksa rasmi kwa Kelvin kucheza Genk. Namuona akitamba Genk akiwa na umri wa miaka 18 tu kwa sababu kuna makinda wengi niliwaona Genk, kama Mjamaica Leon Bailey au Mnigeria Wilfried Ndidi huku Passpoti zao zikionyesha wana miaka 18 tu.
Wakati Kelvin akiwa na miaka 18, Mbappe halisi atakuwa na miaka 22 tu. Nahisi muda si mrefu kuna aibu inaweza kutokea. Itakuwa vipi kama Genk wakipangwa na PSG katika kundi moja la Ligi ya Mabingwa? Hatuwezi kuwa na Mbappe wawili uwanjani.
Huyu Kelvin John ana kil kitu cha kuwa mchezaji kama Mbappe katika siku za usoni. Kama si kumfikia Mbappe basi walau kufika katika uwezo wa Mbwana Samatta. Kama akifikia uwezo wa Samatta pale Genk, na wengi tunaamini hivyo kwa sababu ana makali na amekwenda katika umri mwafaka, itakuaje tuwe na Mbappe wawili uwanjani.
Kwa mfano, ingekuwa vipi Mbwana Samatta angekuwa anajiita ‘Lallana’? ina maana majuzi hapa tungekuwa na Lallana wawili uwanjani katika pambano la Ligi ya Mabingwa wa Ulaya kati ya Genk na Liverpool. Vipi kama Samatta angejiita Milner? Tungekuwa na Milner wawili uwanjani.
Majina ya bandia ya mastaa wakubwa inabidi wapewe wachezaji waliopishana umri kwa kiwango kikubwa. Kelvin John na Mbappe wamepishana miaka minne tu na huyu Kelvin wetu ana mwelekeo wa kuwepo uwanja mmoja na Mbappe muda si mrefu kuanzia sasa.
Kama Kelvin John angekuwa anaitwa Ronaldo ningeweza kuelewa. Ronaldo anaishia zake. Sioni kama ana muda mrefu wa kukutana na Kelvin John uwanjani. Huyu Mbappe watakutana. Mungu atajalia na watakutana haraka iwezekanavyo.
Waghana walimuita Abeid Ayew jina la Pele miaka mingi baada ya Pele halisi kuondoka katika soka. Hawakuweza kukutana kwa hiyo sio jambo la kushangaza sana. Wapo walioitwa lakini tofauti ya miaka haikuwakutanisha.
Lakini pia kumbukumbu zinanionyesha kwamba wachezaji wenye uwezo mkubwa majina ya wachezaji wengine huwa yanawakataa. Sijui itakuwaje kwa Kelvin John lakini hata Samatta hakuweza kupewa jina la staa mwingine kwa sababu uwezo wake binafsi ulikuwa unajipambanua wenyewe.
Ni jukumu la makinda wengine kuitwa Samatta baada ya uwezo aliouonyesha. Zamani kuliibuka na akina Mogella wengi mitaani lakini hawakuwa na uwezo huo ndio maana majina yao yakapata kifo cha asili wakatokomea kusikojulikana.
Kitu kingine ambacho wenzetu wanafanya kwa ajili ya kuepusha Mbappe wawili kukutana uwanjani ni kujaribu kutoa majina yaliyo nje ya soka lakini ambayo yanalingana na uwezo wa mchezaji. Lionel Messi anaitwa La Pulga. Waargentina hawakuweza kumuita Maradona licha ya tofauti kubwa ya umri baina yao kwa sababu Messi alikuwa anajipambanua kama Messi.
Waamerika Kusini ni mabingwa wa majina mbadala lakini mengi yameegemea katika eneo analotoka au kitu fulani chenye maajabu. Juan Sebastian Veron walimuita ‘La Brujita’ wakimaanisha ‘Mchawi mdogo’.
Pale Ireland Kaskazini waliwahi kutoa mmoja kati ya wachezaji bora wa muda wote duniani. Aliitwa George Best. Jina pekee waliloweza kumpa ni Belfast Boy kwa sababu alikuwa amezaliwa katika mji mkuu wa nchi hiyo Belfast. Ni kama vile umuite Samatta kwa eneo lake ‘Mbagala Boy’.
Tungepunguza kumuita Kelvin John jina la Mbappe na kufanya utaratibu mwingine unaoendana na aina yake ya mchezo na tutegemee atakuwa na hadhi kubwa inayokaribiana na Mbappe ndani ya miaka michache ijayo.
Unaweza kudhani natania lakini namuona Kelvin John mbali zaidi. Maamuzi ya kwenda Ulaya kwa sasa yanaweza kumpeleka mbali kuliko huku ambako Mbwana Samatta amefika. Mbappe atakapofika miaka 28 akiwa amepamba moto, Kelvin anaweza kuwa na miaka 24 akiwa amepamba moto na anasakwa Ulaya nzima.

Advertisement