Coastal Union, Lipuli, Kagera wagombea nafasi za Yanga, Azam Ligi Kuu Tanzania Bara

Muktasari:

Ushindi wa timu hizo utazifanya Yanga na Azam kupoteza nafasi zao wakati huu wakiwa katika Kombe la Mapinduzi Zanzibar na kesho Alhamisi timu hizo mbili zitacheza mechi za nusu fainali ya mashindano hayo kwenye Uwanja cha Amaan.

Dar es Salaam.Mabingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara 1988, Coastal Union na Lipuli FC leo zitakuwa na nafasi kubwa ya kuzishusha Yanga na Azam katika msimamo wa ligi hiyo.

Coastal Union chini ya kocha Juma Mgunda itakuwa na kibarua kizito nyumbani Mkwakwani dhidi ya Kagera Sugar inayoshika nafasi ya sita katika msimamo wa ligi hiyo.

Coastal Union inayoshika nafasi ya tatu ikiwa na pointi 26, iwapo watashinda leo watafikisha pointi 29 na kuwachomoa Azam waliokuwa katika nafasi ya pili na pointi 26.

Kagera Sugar waliokuwa kwenye nafasi ya sita na pointi 24, kama wakifanikiwa kumfunga Coastal Union watafikisha pointi 27, nao kupanda mpaka kwenye nafasi ya pili kwenye msimamo wa ligi huku wakisikilizia matokeo ya Lipuli.

Lipuli inayoshika nafasi ya tano wakiwa na pointi 24, watakuwa ugenini kucheza dhidi ya KMC, kama watashinda watafikisha pointi 27, itakayowafanya wapande kwa nafasi tatu hadi nafasi ya pili huku wakisikilizia matokeo ya Coastal Union ambao watacheza na Kagera Sugar.

Ushindi wa timu hizo utazifanya Yanga na Azam kupoteza nafasi zao wakati huu wakiwa katika Kombe la Mapinduzi Zanzibar na kesho Alhamisi timu hizo mbili zitacheza mechi za nusu fainali ya mashindano hayo kwenye Uwanja cha Amaan.

Michezo mingine leo itawashuhudi Mbeya City wenye pointi 10, wakiwa nafasi ya 18, watakuwa  kwenye uwanja wao wa nyumbani wa muda wa Samora Iringa kucheza dhidi ya Namungo inayonafasi ya nane wakiwa na pointi 22.

Katika uwanja wa Nyamagana Mwanza wenyeji Alliance wakiwa nafasi ya 12, wakiwa na pointi 20, wataikaribisha JKT Tanzania inayoshika nafasi tisa na pointi 22.

Mwadui ya Shinyanga wakiwa nafasi ya 15, wakikusanya pointi 16, watakuwa nyumbani kucheza dhidi ya Ruvu Shooting iliyo nafasi ya 13, wakiwa na pointi 19.

Mechi ya sita itakuwa kati ya Polisi Tanzania watakuwa nyumbani uwanja wa Ushirika Moshi kucheza dhidi ya Biashara United ya Mara.  Mechi zote zitachezwa saa 10:00, jioni.