Ukweli Ndivyo Ulivyo! Mwacheni tu Ramos aimbiwe ‘hepi Bethdei’

Sunday April 5 2020

Mwanaspoti, Ukweli Ndivyo Ulivyo, Tanzania, Mwacheni tu Ramos, aimbiwe ‘hepi Bethdei’, Real Madrid, Hispania

 

By Badru Kimwaga

JUMATATU ya wiki hii, kuna kidume kimoja kule Hispania kilikuwa kinaadhimisha miaka kadhaa tangu kuzaliwa kwake. Naamini wazazi wake wanajivunia kuzaa kidume hiki. Kidume jeuri na kibabe kwelikweli. Kidume kinachowanyima raha wanaume wenzake uwanjani.
Ndio, Sergio Ramos alikuwa akiadhimisha miaka 34 tangu kuzaliwa kwake. Alizaliwa Machi 30, 1986. Hapa tunauzungumzia umri sahihi wa beki huyo wa kati wa Real Madrid na Hispania. Sio umri wa nyota wa Kiafrika, ambao wakikuambia wana umri wa miaka 34, lazima nawe uongeze miaka mingine kuanzia mitano ili kupata umri halisi wa wahusika.
Kwa umri alionao Ramos na kazi kubwa aliyoifanya uwanjani, ni wazi hana alichopoteza. Ramos ni mmoja wa mabeki visiki na wenye roho mbaya. Mabeki wenye uwezo mkubwa wa kukaba na vilevile kufunga mabao. Mabeki wa aina hii kwa Tanzania ni wachache na pengine hawapo kabisa tangu aondoke, Nadir Haroub ‘Cannavaro’. Beki wa kati anapaswa kuwa na roho mbaya kwelikweli. Beki anapaswa kuogopwa na washambuliaji. Tanzania ya leo ina mabeki laini. Mabeki wanaoshindana kuweka viduku na kuposti picha kwenye instagramu wakati akila chips na mayai.
Wale wala ugali wa dona na mandondo. Wale ambao asubuhi wanapiga bakuli za kutosha za uji wakisukumia na buruga hawapo tena.
Hata hawa kina Kelvin Yondani, Juma Said Nyosso, Aggrey Morris wanaotajwa kama mabeki wenye kariba hiyo, nao wanaondoka na soka lao. Hawana rekodi tamu za kusisimua, lakini wao ni angalau kidogo.
Ukweli ulivyo, huwa natamani sana kuona siku moja Tanzania nayo inakuwa na mabeki aina ya Ramos. Bakar Malima ‘Jembe Ulaya’ na hata Nadir Haroub ‘Cannavaro’ alijitahidi, ila hawajafikia hata robo ya Ramos, ila nawapa heshima yao. Utamu ni licha ya Ramos kuwa beki, lakini jamaa ana mabao mengi kuliko hata baadhi ya mastraika wenye kazi ya kufunga uwanjani dhidi ya timu pinzani.
Kama nahodha wa Real Madrid kuna wakati amekuwa akijitoa kuhakikisha kila kitu kinaenda sawa. Hivi ndivyo nahodha anapaswa kuwa. Kuiongoza na kuibeba timu mabegani. Kwa hapa Tanzania kwa kizazi cha sasa sijaona. Huu ndio ukweli. Tusidanganyane. Achana na undava wake ambao wakati mwingine umekuwa ukiigharimu timu, angalia mchango wake ulioibeba Real na hata tuimu yake ya taifa ya Hispania.
Achana na kadi zake zaidi ya 20 nyekundu kwa mashindano yote akiwa ndiye kinara, we angalia alivyozisaidia timu zake kwa kuokoa mabao, pia amekuwa akifunga magoli muhimu dhidi ya wapinzani wao. Aina yake ya uchezaji ni wazi imeacha kumbukumbu kwa Mohamed Salah. Salah na Liverpool nzima wanamkumbuka beki huyo. Huenda Liverpool bado wana hasira naye kama ilivyokuwa kwa Wamisri waliochukizwa na kile aliochowafanyia kueleka Fainali za Afcon 2019.
Wamisri walikuwa wanajiandaa na fainali hizo kama wenyeji, lakini kidume hicho kikawatibulia kwa kumjeruhi Salah kwenye fainali za Ligi ya Mabingwa Ulaya 2018 na Real Madrid kutwaa taji kwa ushindi wa mabao 3-1.
Mashabiki wanaamini kuumia kwa Salah ambaye hata hivyo alijitutumua na kuchezeshwa akiwa hajawa fiti kwa kiasi kikubwa ilichangia Misri kupata aibu kwa kuaga mapema na kuwaachia majirani zao Algeria kutakata kwa kulitwaa taji hilo wakienda kuifunga Senegal katika fainali.
Ukiangalia umri wake wa miaka 34 tena kama beki, Ramos ana rekodi tamu kuliko hata baadhi ya nyota unaowafahamu. Wapo baadhi ya nyota mbalimbali ulimwenguni, hawajawahi kubeba Kombe la Dunia, akiwamo Lionel Messi na hata Cristiano Ronaldo, lakini Ramos kabeba. Kuna mastaa kibao hawajawahi kunyakua ubingwa wa Ligi ya Mabingwa Ulaya, lakini kidume hiki kimebeba mara nne. Hapo sikuambii Klabu Bingwa ya Dunia alilobeba mara nne, UEFA Super Cup mara tatu, ubingwa wa Euro Cup (2), La Liga (4) na Copa del Rey (2).
Katika mechi 444 katika La Liga jamaa katupia mara 64 na ukijumuisha mechi zake zote za ligi tangu anapoibuka kwenye Sevilla B, Ramos amecheza jumla ya mechi 716 za mashindano yote akiwa na klabu alizochezea ikiwamo Sevila na Real Madrid akifunga mabao 96. Ni mabao mengi kwelikweli kwa mchezaji wa nafasi yake.
Kama unadhani jamaa kufunga anabahatisha, we chungulia rekodi yake katika timu ya taifa ya Hispania aliyoanza kuichezea tangu mwaka 2005, kwani amefunga mabao 21 katika mechi 170.
Ukiacha kadi zake zake nyekundu, Ramos pia amevuna kadi za njano za kutosha, zikiwa ni zaidi ya 160 na kumfanya awe mchezaji asiyejutia chochote.
Ndio, ajute nini wakati kama mataji ya ubingwa anayo? Mabao pia anayo. Na hata rekodi ya kadi anazo, mbali na ubabe wake unaomfanya awe anaogopwa na baadhi ya nyota wa timu pinzani.
Naamini kwa rekodi hizo za kidume hicho, bila ya shaka kwa wachezaji wanaocheza sasa nchini na wale wanaochipukia kuna kitu cha kujifunza kutoka kwake. Soka ni mchezo wa wanaume. Wanaume wanaojitoa kwselikweli ili kuyafikia mafanikio.
Ramos alijitoa kwelikweli kwa miaka yake karibu 17 ya kusaka soka. Ndio maana sioni sababu kwa nini kidume hiki, kisiimbiwe lile songi ‘Happy Birthday...! 

Advertisement