Simba SC yajifua Uwanja wa Kirumba, Sven aiwaza Stand United

Muktasari:

Simba ilitua leo alfajiri ikitokea jijini Dar es Salaam imefanya mazoezi kwenye Uwanja wa CCM Kirumba Mwanza kujiandaa na mchezo wa Kombe la FA dhidi ya Stand United, utakaopigwa Kambarage mjini Shinyanga Jumanne.

Mwanza. Kocha Simba, Sven Vandenbroeck amesema anawaheshimu wapinzani wake Stand United na wanaenda kwa umakini kuhakikisha wanashinda mechi hiyo ya Kombe la Shirikisho Azam.

Simba itashuka uwanjani Jumanne ijayo kuwakabili Stand United katika mchezo wa kusaka kufuzu kwa robo fainali ya Kombe Shirikisho Azam utakaochezwa kwenye Uwanja wa Kambarage mjini Shinyanga.

Akizungumza jijini Mwanza kabla ya kuanza kwa mazoezi Sven amesema kikosi chake kipo fiti wanawafuata wapinzani wao kwa umakini ili kupata ushindi na kusonga mbele.

"Tumepata ushindi katika mechi zetu takribani nne, lakini lazima tuwe makini kuwakabili Stand United kwa sababu siwajui vizuri malengo yetu ni kushinda na vijana wangu wako fiti," amesema kocha huyo.

Licha ya Kocha huyo Mbelgiji kuwataja, Miraji Athuman na Mzamiru Yassin kutokuwapo katika kikosi kutokana na majeruhi, Mwanaspoti imejidhisha nyota wengine kutokuwapo katika mazoezi ya leo na habari za ndani ni kuwa huenda hata mechi ya Jumanne wakakosekana.

Nyota hao ni Kipa, Aish Manula, Kiungo Luis Miquissone, mabeki Shomari Kapombe,  Mohamed Hussien 'Tshabhalala' na Erasto Nyoni, ambao mchezo uliopita dhidi ya Biashara United walicheza.

Hata hivyo, wakati wachezaji wakiendelea mazoezi, nyota watano wameonekana wakijifua peke yao, ikiwa ni Meddie Kagere, Clatous Chama, Jonas Mkude, Francis Kahata na Paschal Wawa.

Mwanaspoti ambayo ilikuwa uwanjani hapo kuanzia mwanzo hadi mwisho, iliwashuhudia nyota hao wakikimbia uwanja zaidi ya mara tano kisha kuanza kujinyoosha viungo.

Baada ya mazoezi ya leo Jumapili jioni, Wekundu hao wataondoka kesho asubuhi Jumatatu kuelekea mjini Shinyanga tayari kwa ajili ya mpambano huo.