Mmesikia...eti Ozil hatakiwi Arsenal

Friday September 20 2019

 

LONDON, ENGLAND. BEKI wa pembeni wa zamani wa Liverpool, Glen Johnson amesema sasa rasmi anafahamu kwamba kiungo Mesut Ozil hatakiwi Arsenal.
Mjerumani huyo, Ozil hakujumuishwa kwenye kikosi cha Arsenal kilichosafiri kuifuata Eintracht Frankfurt kwenye mikikimikiki ya Europa League juzi Alhamisi.
Johnson alisema akiambia talkSPORT: "Wachezaji wanapopumzishwa, basi wanapumzishwa wakiwa kwenye benchi.
“Hivyo, wanaweza kukosa dakika 80 za mchezo, lakini wanakuwapo kwenye msafara wa timu na kuwekwa kwenye benchi. Hapo unakuwa bado upo kwenye mipango ya timu, unawapa sapoti wachezaji wenzake, huwezi kujua, pengine unaweza kuhitajika kwenye dakika 10 za mwisho.
“Lakini, Ozil hakusafiri na timu na hapo huwezi kusema kwamba umempumzisha, kuna kitu cha zaidi kwenye hilo."
Ozil, ambaye analipwa mshahara mkubwa zaidi huko Arsenal, mkataba wake utafika tamati 2021, huku akiwa anapokea Pauni 350,000 kwa wiki licha ya kocha Unai Emery kumchezesha kwa dakika 71 tu msimu huu.
“Huwezi kuwaacha tu wachezaji, hasa wachezaji wako wakubwa, unawacha nyumbani," alisema Johnson na kuongeza. “Hasa ukizingatia kwamba alifanya mazoezi, hukuunaondoka na makinda watano, hakuna anayefanya hivyo. Inaumiza usiposafiri na timu, lakini inaumiza zaidi kama unafanya mazoezi na wenzake na kisha wenzake wanatumika kwenye mechi, wewe unawekwa pembeni. Si wachezaji wote wanaweza kukabiliana na hilo."
Kocha Emery amekuwa hana mipango na Ozil, huku staa huyo aliripotiwa kuwekwa sokoni kwenye dirisha lililopita la usajili na shida ni kwamba hakukuwa na timu iliyokuwa tayari kumsajili kutokana na mshahara wake kuwa mrefu.

Advertisement