Mhilu, Lusajo wamkomalia Kagere

Wednesday March 18 2020

Mhilu, Lusajo wamkomalia Kagere,ubingwa wa Ligi Kuu Bara,tuzo ya kiatu cha dhahabu,Mwanasport,

 

By Olipa Assa

ACHANA na mbio za kuwania ubingwa wa Ligi Kuu Bara ambao kimahesabu Simba inasubiri kukabidhiwa tu na ile bato ya kujinusuru kushuka daraja, ishu kali ni nani ataibuka mfumania nyavu bora na kubeba tuzo ya kiatu cha dhahabu.

Kuna vita ya straika matata wa Simba, Meddie Kagere na wazawa ambao hawataki kubaki nyuma wakimfukuzia Mnyarwanda huyo mwenye mabao 19, lakini halijawanyima raha akina Yusuf Mhilu wa Kagera Sugar na Reliants Lusajo anayekipiga Namungo FC.

Jamaa wamegoma kunyoosha mikono kwa Kagere na kuamua kukomaa naye mwanzo mwisho hadi dakika ya mwisho, ambapo wamesema lolote linaweza kutokea.

Akizungumza na Mwanaspoti jana, Mhilu alisema anapata kigugumizi kung’amua kama anaweza akamfukuzia Kagere.

Mhilu mpaka sasa ana mabao 11 ndiye kinara wa mabao kwenye timu ya Kagera Sugar, alisema amezidiwa mabao nane, ingawa soka ni mchezo wa maajabu lolote linaweza likatokea hata kama ni mzunguko wa pili.

“Mfano yeye mwenyewe Kagere hakufunga muda mrefu akaja akaibukia kwa Singida kufunga mabao manne, hilo ndilo linanifanya nisikate tamaa kwamba ninaweza nikafanya maajabu, ingawa naona ana nafasi kubwa,” alisema.

Advertisement

straika wa Namungo FC, Reliants Lusajo anayemiliki mabao 11 alisema bado kuna mechi nyingi hivyo hawezi kunyosha mikono kumwachia Kagere kwamba ndiye atakuwa mfungaji bora.

“Ni changamoto kuzidiwa na wageni ingawa kuna wakati hata sisi wazawa tunafanya vyema, binafsi inanipa taswira ya kujituma kwa bidii, sijakata tamaa nitapambana mpaka nukta ya mwisho,” alisema.

mshambuliaji wa Mbeya City, Peter Mapunda ambaye anamiliki mabao tisa, alisema licha ya kuzidiwa mabao 10 na Kagere anaamini wazawa wanaweza wakachukua kiatu hicho. Wazawa wengine ambao wanaongoza kwa mabao mengi ni Paul Nonga wa Lipuli ana mabao 11, Daruwesh Saliboko ana nane na Ayubu Lyanga kutokana Coastal Union ana nane.

Advertisement