Messi aingilia dili la Neymar Barcelona

Wednesday August 14 2019

 

Barcelona, Hispania. BADO kuna utata mkubwa wa mahali ambako supastaa wa Kibrazili, Neymar atakapokuwa msimu huu. Real Madrid, Barcelona na PSG zote zinataka huduma yake.

Hata hivyo, habari za kuaminika ni kuwa nahodha wa Barcelona, Lionel Messi ambaye ni mshkaji wa karibu na Neymar ameamua kuingilia kati dili hilo kuhakikisha anaungana tena na Mbrazili huyo.

Inaelezwa kuwa, Messi amempigia simu Neymar akimtaka kuachana na mpango wa kwenda Madrid na badala yake arejee Catalunya ili wakauwashe moto kwa mara nyingine.

Messi na Neymar walikuwa na msimu mzuri pale Barcelona wakiunga kombinesheni matata sambamba na Luis Suarez iliyopewa jina la MSN ambayo ilikuwa inafunga mabao itakavyo.

Neymar aliachana na Barcelona kwenda zake PSG mwaka 2017, akiweka rekodi mpya ya dunia ya uhamisho wa pauni 189 milioni, lakini sasa amedai hana furaha na maisha ya Jiji la Paris.

Licha ya kushinda mataji mawili mfululizo ya League 1, Neymar ameeleza dhamira yake ya kuachana na wababe hao ili kurejea zake Hispania.

Advertisement

Messi, ambaye amekuwa mchezaji mwenye nguvu ya kuamua mchezaji gani asajiliwe ndani ya kikosi hicho, amepanga kuzungumza na Rais wa Barcelona, Josep Maria Bartomeu kuhakikisha dili la Neymar kurejea linatimia.

Advertisement