Mechi mbili za kuzigawa Simba, Yanga Ligi Kuu

Muktasari:

Yanga itacheza na Kagera, wakati Simba ikiialika Biashara

 

Dar es Salaam. Mechi mbili za ugenini dhidi ya Kagera Sugar na Mtibwa Sugar ni mtihani mgumu kwa Yanga unaoweza kuipa nguvu kubwa au kuitibulia hesabu katika mbio za ubingwa wa Ligi Kuu Kuu msimu huu.

Ugumu wa kucheza katika viwanja vya mikoani, historia ya ushindani ambao Mtibwa na Kagera Sugar zimekuwa zikitoa dhidi ya timu kubwa na matokeo ya mechi mbili za mwanzo za ligi kwa kila timu, vyote vinailazimisha Yanga kuingia kwa tahadhali.

Baada ya kucheza mechi mbili za mwanzo Uwanja wa Benjamini Mkapa jijini na kuvuna pointi nne, nyota wapya wa Yanga watakuwa na kibarua cha kuonja viwanja vya mikoani, ambavyo kiubora havifanani na ule walioutumia katika mechi za ufunguzi dhidi ya Tanzania Prisons na Mbeya City.

Angalau Yanga wanaweza kupata mteremko dhidi ya Kagera Sugar Septemba 19 kutokana na Uwanja wa Kaitaba kuwa wa nyasi bandia, ambao hauwezi kuwaathiri sana kwani wamekuwa na uzoefu na matumizi ya viwanja vya namna hiyo.

Lakini baada ya mchezo huo, Yanga itaelekea Morogoro kuikabili Mtibwa Sugar katika Uwanja wa Jamhuri, ambao umekuwa hauna eneo zuri la kuchezea na itawalazimu kuwa na mbinu zaidi uwanjani

Ni Uwanja huo wa Jamhuri ambao katika mchezo uliopita, nyota wa Simba, ambao wamekuwa wakisifika kuwa na kiwango bora, walishindwa kuhimili ubora wa eneo la kuchezea na kujikuta wakifunikwa na wenzao wa Mtibwa.

Ukiondoa hilo, jambo lingine linaloipa ugumu Yanga katika mechi hizo ni matokeo yasiyoridhisha, ambayo Mtibwa na Kagera Sugar waliyapata katika mechi mbili za mwanzoni, yatazifanya zijipange vilivyo kwa ajili ya mechi hizo kwa kufanyia kazi mapungufu yao.

Katika mechi mbili za kwanza, Kagera Sugar ilianza kupoteza nyumbani kwa bao 1-0 dhidi ya JKT Tanzania na mechi iliyofuata ilitoka suluhu na Gwambina FC ugenini, wakati Mtibwa yenyewe ikitoka sare katika mechi zake mbili nyumbani dhidi ya Ruvu Shooting na Simba.

Lakini kingine ni historia ya ushindani ambayo timu hizo zimekuwa nayo pindi zikutanapo na Simba ama Yanga.

Ingawa Yanga imekuwa na rekodi nzuri ya kuibuka na ushindi katika mechi walizokutana, msimu uliopita walishangazwa kwa kuchapwa mabao 3-0 nyumbani kwenye Uwanja wa Uhuru na licha ya Yanga kulipa kisasi kwa kushinda bao 1-0 ugenini mkoani Kagera, walikutana na ushindani wa hali ya juu ndani ya dakika 90 kwenye mchezo huo.

Kocha wa Yanga, Zlatko Krmpotic alisema hesabu zake ni kukusanya pointi sita katika mechi hizo ngumu mbili zilizo mbele yake.

“Nina imani kila siku zinavyozidi kwenda, kikosi kitakuwa imara, sasa akili yetu inajiandaa na mechi zijazo, tutahakikisha pia tunapata alama zote muhimu katika mechi hizo,” alisema.

Kocha wa Mtibwa Sugar, Zubery Katwila alisema kuwa timu yake inaupa uzito sawa mchezo dhidi ya Yanga kama ilivyo kwa mingine.

“Tunawaheshimu Yanga, lakini siku zote historia haina nafasi kubwa katika mchezo wa soka. Jambo la muhimu ni kujiandaa vizuri na kufanyia kazi mapungufu yetu tuliyoonyesha katika mchezo uliopita.

Kwa maana ya uzito, mechi zote za ligi zina thamani ile ile na hakuna cha kusema hii mechi kubwa au ndogo,” alisema Katwila.

Wakati hali ikiwa hivyo kwa Kagera Sugar, Mtibwa ndio imekuwa ikimsumbua vilivyo Yanga pindi wakutanapo katika Ligi Kuu na ushahidi wa hilo ni matokeo ya mechi tano za mwisho zilizokutanisha timu hizo, kila upande umeibuka na ushindi mara mbili na kutoka sare moja.

Hali ikiwa hivyo kwa Yanga, watani zao Simba wanarejea jijini kucheza mechi mbili dhidi ya Biashara United na Gwambina, huku wakibebwa na ubora wa uwanja, takwimu nzuri za kushinda nyumbani na ugeni wa mazingira kwa wapinzani wake hao.

Simba haijawahi kupoteza mchezo dhidi ya Biashara United, wakati Gwambina FC ikicheza kwa mara ya kwanza kwa Mkapa.