Mchongo wa Mwanaspoti wazidi kumwaga zawadi

Muktasari:

Katika droo hiyo ya tano, washindi wengine sita walijinyakua zawadi tofauti akiwamo Salenja Hashim wa Magomeni Mwembechai aliyeshinda simu janja (smartphone) huku wenzake watano wakinyakua kitita cha Sh100,000 kila mmoja.

PROMOSHENI ya Shinda Mchongo wa Mwanaspoti imeingia wiki ya tano kwa washindi mbalimbali kujinyakulia zawadi na kwa mara nyingine Bodaboda imeenda tena kwa mkazi wa Dar es Salaam baada ya Cosmas Elias mkazi wa Ubungo ambaye ni muuza nyama kunyakua zawadi hiyo mchana huu.
Cosmas aliliambia Mwanaspoti mara alipopigiwa simu kufahamishwa juu ya ushindi wake, kuwa zawadi hiyo imempa mzuka wa kucheza zaidi promosheni hiyo, lakini ameanza mipango mingi ya kuitumia kumuingizia kipato zaidi mbali na shughuli zake za buchani.
"Nilikuwa nacheza kila nikinunua gazeti la Mwanaspoti na ninathubutu kusema promosheni hii imebadilisha mfumo wangu wa kupata kipato kimaisha na kwenda kunisaidia katika kuendesha familia yangu katika mazingira salama zaidi," alisema Elias.
Elias anakuwa mshindi wa tatu wa Bodaboda kutokea jijini Dar es Salaam, baada ya wengine wawili akiwamo Giziraly Malibiche wa Temeke  na Wilfred Magige wa Magomeni Mikumi kubeba katika droo nne zilizopita.
Katika droo hiyo ya tano, washindi wengine sita walijinyakua zawadi tofauti akiwamo
Salenja Hashim wa Magomeni Mwembechai aliyeshinda simu janja (smartphone) huku wenzake watano wakinyakua kitita cha Sh100,000 kila mmoja.
Waliovuta mkwanja huo wa Sh100,000 kila mkoja ni Joel Sahaye kutoka Iringa, Seleman Michaka anayebana Vingunguti,  Dar es Salaam, Hawa Said wa Visiga Kibaha, Nicholaus George kutoka Tanga na Mazela Ramadhani anayeishia Mwanza.
Promosheni hiyo iliyoanza Julai Mosi, itaendeshwa kwa wiki 12 mpaka Septemba ambapo droo kubwa itafanyika kwa kupatikana washindi wawili watakaogawana Sh10 milioni.