Mbelgiji amzuia Dante Jangwani

BAADA ya kuwepo kwa sintofahamu kwa mashabiki wa Yanga kuona beki wao Andrew Vincent ‘Dante’ anasugua benchi, mchezaji huyo ameamua kufunguka na kuelezea sababu, huku Kocha Luc Eymael akieleza kuwa bado anamhitaji beki huyo wa kati kikosini hapo.

Dante aliliambia Mwanaspoti kwamba hakuna mchezaji, ambaye anapenda kuwa mtazamaji wakati wenzake wanafanya kazi, sababu anayoiona kwa nini hachezi ni ugeni wa Eymael tu.

Alifafanua kauli yake, alisema kutokana na kukaa nje kwa muda mrefu takribani miezi minne, kumemfanya Eymael amuone mgeni kwenye kikosi chake.

Pamoja na changamoto hiyo, Dante alisema haimfanyi ashindwe kutimiza majukumu yake anapokuwa mazoezini na uwanjani.

“Kama mazoezi nafanya kwa bidii kwa sababu najitambua kuwa soka ni kazi yangu, kocha ndiye mwenye uamuzi wa nani amtumie kutokana na mbinu zake hivyo, siwezi kumwambia mimi ndiye nastahili nipange mwache fulani hapa,” alisema Dante na kuongeza;

“Pia nimekaa muda mrefu nikiwa nje ya kazi, nilijiunga na timu kama sikosei ilikuwa Novemba, ndio maana nimesema labda ugeni wa kocha, nje na hapo naendelea kupambana kufanya kile ninachoona nastahili kukifanya,” alisema.

Wakati Dante akisema hayo huku mkataba wake ukielekea ukingoni na inaelezwa kuwa Eymael amesema anapenda kuona beki huyo anabaki kikosi japo hakuweza kufafanua zaidi kuhusu mipango yake ya msimu ujao.

“Kukosa nafasi kwa Dante kumetokana na kukosekana muda mrefu kikosini hivyo, anatakiwa aonyeshe kupitia mechi atakazopewa, tayari nimeanza kumwingiza kwenye kikosi. Siwezi kusema zaidi kuhusu msimu ujao ila namuhitaji ili asaidiane na wenzake,” alisema Eymael

KAULI ZA

WADAU

Winga wa zamani wa Simba, Emmanuel Gabriel alisema kufanya vyema kwa wachezaji wazawa kwenye klabu zao kutaleta matunda katika timu ya taifa na kwamba, bado anaamini Dante ni mchezaji mzuri ila anapaswa kusubiri mipango ya kocha wake.

“Kocha ndiye msemaji wa mwisho wa wachezaji, lakini kama hana tatizo lolote basi ni changamoto kwa timu yetu ya taifa maana ndio vijana wenyewe wanaotegemewa, mengine tunaachia benchi lake la ufundi,” alisema.

Mchezaji wa zamani wa Yanga, Ally Mayay amesema usimamizi mbaya wa wachezaji umekuwa ni chanzo cha wachezaji wengi kushusha viwango vyao na kuweka wazi kuwa suala la Dante kukaa nje ya uwanja kwa sasa limechangiwa na changamoto ya madai dhidi ya Yanga. “Kuna utaratibu mzuri wa kudai ukiwa bado unapambania kipaji chako, ikitokea umelipwa unakuwa tayari uko vizuri ila kwa Dante ilikuwa tofauti na kutoa nafasi kwa engine kuonyesha na kukuza viwango,” alisema Mayay.

Imeandikwa na Olipa Assa, Charity James na Thomas Ng’itu