Mbappe aomba kuuzwa kwenda Madrid

Thursday June 6 2019

 

PARIS,UFARANSA.NAAM inaonekana itakuwa kivumbi na jasho katika dirisha hili la uhamisho. Habari za chini chini kutoka Hispania zinadai kwamba staa wa PSG, Kylian Mbappe ameandika barua ya kuomba kuuzwa na PSG ili akamilishe uhamisho wa kwenda Real Madrid.

Madrid inaonekana kupania kununua mastaa katika dirisha hili la uhamisho baada ya kufungua pochi kubwa kwa mara ya mwisho mwaka 2013 wakati walipomnasa staa wa kimataifa wa Wales, Gareth Bale kutoka Tottenham.

Mapema mwezi uliopita, Mbappe, 20 alikiri kuwa huenda angetimka klabuni hapo na kwenda kwingineko, na sasa kituo cha cha El Chiringuito kimedai kwamba, staa huyo wa kimataifa wa Ufaransa ameomba kuuzwa.

Taarifa hii imekuja wakati huu ikidaiwa kwamba, Real Madrid wanamtaka staa mmoja kati ya Mbappe au Neymar wakati huu kocha, Zinedine Zidane akiwa amepania kufanya mabadiliko makubwa katika kikosi chake.

Hivi karibuni kocha wa PSG, Thomas Tuchel aliweka wazi kuwa hakuwa na uhakika kama staa huyo angeendelea kubakia klabuni hapo huku ripoti zikidai kwamba, wawili hao walikuwa wana matatizo.

“Kama kocha, nataka waendelee (Mbappe na Neymar) lakini hili ni soka. Klabu nyingi zinataka kununua wachezaji na kwa sasa soko la wachezaji kama vile lina wazimu, lakini ukiniuliza kama kocha nitakwambia nataka waendelee kukipiga hapa msimu ujao. Lakini kama hawatakuwepo tutatafuta mbinu nyingine,” alisema Tuchel.

Advertisement

Wakati Tuchel akizungumza hayo, Mbappe alionyesha kutokuwa na uhakika na hali yake ya baadaye klabuni hapo na akizungumza mara baada ya kupokea tuzo ya mchezaji bora wa msimu alikiri kuwa katika hali hiyo.

“Ni kitu muhimu kwangu, nimefika katika kipindi muhimu cha maisha yangu ya soka. Nimegundua mengi hapa, na nadhani ni kipindi ambacho inabidi nibebe majukumu zaidi. Nadhani hilo linaweza kuwa PSG , itakuwa vizuri, au inaweza kuwa kwingineko ambako kuna mradi mpya,” alisema Mbappe.

Madrid inaonekana kupania kujenga upya kikosi chao msimu huu baada ya kumpoteza Cristiano Ronaldo aliyekwenda Juventus katika dirisha lililopita, lakini pia wamepoteza taji lao la Ulaya walilotwaa mara tatu mfululizo na safari hii limechukuliwa na Liverpool.

Tayari wametangaza kumnasa mshambuliaji nyota wa kimataifa wa Serbia, Luka Jovic kutoka klabu ya Eintracht Frankfurt ya Ujerumani na staa huyo amesaini mkataba wa miaka sita huku ikiwa ni kiashiria cha mwisho wa staa wao wa kimataifa wa Ufaransa, Karim Benzema.

Madrid pia wapo katika dakika za mwisho kumnasa staa wa kimataifa wa Ubelgiji, Eden Hazard kutoka Chelsea huku dili hilo likikaribia kukamimilika na litamuona Hazard akitua Santiago Bernabeu kwa dau la pauni 115 milioni.

Staa mwingine ambaye anaweza kutua klabuni hapo katika dirisha hili ni kiungo wa kimataifa wa Ufaransa wa Manchester United, Paul Pogba ambaye inadaiwa yuko tayari kupunguzwa sehemu ya mshahara wake ili aende Santiago Bernabeu.

Kuna mastaa ambao wanatazamia kupisha njia kwa wachezaji wengine. Nyota Gareth Bale ambaye alinunuliwa kwa mbwembwe na Madrid mwaka 2013 kwa rekodi ya uhamisho ya dunia ameambiwa wazi na Zidane kwamba, hayupo katika mipango yake na ni wazi anaweza kurudi England.

Wengine ambao watapisha njia kwa Madrid mpya ni pamoja na kiungo wa kimataifa wa Colombia, James Rodriguez aliyecheza kwa mkopo wa misimu miwili Bayern Munich, lakini klabu hiyo ya Ujerumani imeamua kutomchukua na sasa anaweza kuelekea England au Italia. Kipa Keylor Navas pia anaweza kuondoka klabuni hapo.

Advertisement