Mbappe, mshale wa sekunde unaosogea pale Bernabeu

Muktasari:

Povu la Leonardo lilikuja baada ya Kocha wa Real Madrid, Zinedine Zidane kudai Mbappe ana ndoto za kuichezea Real Madrid. Nilitabasamu. Nilimuonea huruma Leonardo na maumivu anayoyapata. Ataendelea sana kuyapata. Mwisho wa maumivu ni pale Mbappe akisaini Real Madrid.

MAUMIVU? Ndio, maumivu. Aliyasikia mtu anayeitwa Leonardo Jumatano iliyopita. Mkurugenzi wa PSG. Mwaka 1994 akiwa staa wa kikosi cha Brazil alimpiga kiwiko kikali kiungo wa Marekani, Tab Ramos katika michuano ya Kombe la Dunia pale Marekani.

Ramos alipasuka fuvu la kichwa chake na alikaa hospitali kwa miezi mitatu na nusu. Inawezekana Ramos hakusikia maumivu makali kama ambavyo mbabe wake Leonardo alisikia Jumatano jioni, na ataendelea kusikia mpaka pale mtu anayeitwa Florentino Perez atakapofungua pochi lake.

Leonardo alisikika akizungumza kuhusu uvumi unaotanda kila siku wa Kylian Mbappe kwenda Real Madrid. “Kusema kweli inachukiza sana. Hii sio mara ya kwanza kutokea. Nadhani sasa ni muda wa maongezi haya kusimama. Mbappe ana mkataba wa miaka miwili na nusu umebaki kwahiyo kuongea kuhusu anachotaka, ndoto zake, kila wakati…..tafadhali tuache kuongea,” alisikika Leonardo.

Povu la Leonardo lilikuja baada ya Kocha wa Real Madrid, Zinedine Zidane kudai Mbappe ana ndoto za kuichezea Real Madrid. Nilitabasamu. Nilimuonea huruma Leonardo na maumivu anayoyapata. Ataendelea sana kuyapata. Mwisho wa maumivu ni pale Mbappe akisaini Real Madrid.

Ni kitu kama kilichojipanga kutoka kusikojulikana. Mbappe ana asilimia zote za kucheza Madrid. Katika lugha ya kawaida ni kwamba anajibu maswali yote ya kwanini asicheze Madrid. Kwanza kabisa, kuna Galactico gani amebakia sokoni zaidi ya Mbappe?

Kama ukiniuliza nitakwambia Mbappe ni zaidi ya Neymar. Ukiuliza asilimia 100 ya mashabiki wa soka duniani kote wangependa kuwa na nani kati ya Mbappe na Neymar basi asilimia 70 wangejibu Mbappe. Ana makali, ana mchango wa moja kwa moja, hana vitu vingi uwanjani kama Neymar lakini ana madhara makubwa na sio bishoo.

Jibu jingine ambalo linajijibu kwa Mbappe kwenda Real Madrid. Kama akipokea ofa kubwa ya pesa kati ya Madrid na Man City atakwenda wapi? Atakwenda Madrid. Timu yenye historia na hadhi kubwa. Timu ambayo inamuweka katika nafasi nzuri ya kutwaa tuzo ya mwanasoka bora wa dunia.

Hakuna mchezaji wa Man City aliyewahi kutwaa tuzo ya mwanasoka bora wa dunia. Lakini hakuna tofauti kati ya timu ambayo atakuwa ametoka na timu ambayo atakuwa amekwenda. Zote mbili, PSG na Man City zimeundwa vema karibuni tu kwa pesa za mafuta. Hazina historia wala hazikaribii historia ya Real Madrid.

Mbappe hawezi kwenda Barcelona kwa sababu ina Lionel Messi. kilekile alichokimbia Neymar ndicho ambacho hawezi kukifuata. Lakini pia Barcelona iko bize kumrudisha Neymar kuliko kushughulika na Mbappe. Inaonekana kuna kitu inachokijua.

Mbappe hawezi kwenda Juventus kwa sababu Juventus haina pesa ya kumnunua Mbappe. Italia kwa sasa ipo katika pesa ya kuchukua wakongwe ambao wanaelekea kumaliza siku zao kama kina Cristiano Ronaldo. Mbappe wa sasa ana thamani ya zaidi Pauni 200 milioni.

Perez anaweza kusaini hundi ya pesa hizo akiwa amefumba macho. Tangu mwaka 2013 hajavunja rekodi ya uhamisho ya dunia. Uhamisho wa Eden Hazard ulikuwa wa kawaida sana kwake. Anahitaji kuishtua dunia na kama akitaka kufanya hivyo basi jina moja tu litajitokeza katika akili yake. Kylian Mbappe. Aende wapi kwingine?

Waingereza na Mbappe sioni kama wana uhusiano. Mbappe ni wa Madrid tu. kwa sababu zile zile za kuwa mchezaji bora wa dunia sioni Mbappe akienda timu za Ligi Kuu ya England. Mchezaji bora wa mwisho wa dunia kutoka Ligi Kuu ya England alikuwa Cristiano Ronaldo mwaka 2008.

Sioni pia kama Waingereza wanaweza kuwa na uwendawazimu wa Perez wa kutoa Pauni 200 milioni kwa mwili mmoja wa mwanadamu. Sioni. Licha ya utajiri wa Manchester United lakini kwa sababu zilezile ambazo zilisababisha washindwe kushindana na Perez katika enzi za kina Luis Figo, Zidane, Ronaldo de Lima na wengineo ndio sababu zile zile ambazo Waingereza watampisha Mbappe aende kwa Perez.