Mayanja asaini mwaka KMC ahaidi makubwa

Wednesday June 26 2019

 

By Thomas Ng'itu

Dar es Salaam. Kocha mpya wa KMC, Jackson Mayanja amesema anataka kuhakikisha timu hiyo inakuwa tishio katika msimu ujao wa Ligi Kuu.

Mayanja amesaini mkataba wa mwaka mmoja akirithi mikoba ya Mrundi Ettiene Ndayiragije aliyetimkia Azam.

Akizungumza baada ya kusaini mkataba huo, Mayanja alisema anataka kutumia vizuri mashindano ya Kagame Cup kutengeneza timu ili ilete ushindani katika ligi pamoja na Kombe la Shirikisho Afrika.

"Mashindano ya Kagame ndio nitajua timu yangu ipoje na kuweza kufanya mfumo wangu uingie, kwa muda huu uliobaki ndio nitafanya mazoezi na vijana wangu lakini hatuendi kuchukua Kombe Kagame bali tunaenda kitumia kama sehemu ya kutengeneza mfumo ili tuwe bora baaadae," alisema.

Mayanja alisema hatarajii kuongeza mchezaji yoyote katika kikosi hicho bali anaweza kuongeza mtu mmoja wa kusaidiana naye katika benchi la ufundi tu.

"Nataka nianze mazoezi mapema na wachezaji wangu ili kuona inakuaje, lakini nataka kutumia wachezaji hawa hawa kwa sababu ni vijana naamini tutafanya vizuri na nawaamini," alisema Mganda huyo.

Advertisement

Aliongeza baada ya kutua katika kikosi hiko cha Kinondoni, akili yake yote ipo hapo na hafikilii mambo ya zamani hasa kwa klabu ya Simba.

"Ni jambo zuri kuiona Simba ikifanya vizuri nina furaha, mafanikio yangu nikiwa Simba ni historia hivi sasa naangalia hapa nilipo kuweza kukitimiza nilichokifanya kule," alisema.

Meya Kinondoni, Benjamin Sitta alisema anawapongeza viongozi wa Bodi kukamilisha kumpata kocha huyo kwani ana imani naye kubwa.

"Mayanja ni kocha mzuri na akiwa kama mchezaji aliweza kucheza kimataifa akiwa na timu ya Uganda, naamini kabisa kwamba atatumia uzoefu wake kuwapa vijana hasa katika haya mashindano ya kimataifa tunayoenda," alisema Sitta.

Aliongeza licha ya kumpa mkataba wa mwaka mmoja kocha huyo, bado atakuwa anashughulikia mpaka upande wa wachezaji wa timu za vijana.

"Tangu alipokuwa Uganda alikuwa anadili na vijana kwahiyo ni muda wetu kwake na yeye kututengenezea programu za vijana, mkataba wake utaongezwa pindi ukimalizika na tukiona kwamba amefanya kile tunachokihitaji," alisema.

Mayanja sio mgeni na soka la Tanzania baada ya kuzifundisha klabu za Coastal Union, Kagera Sugar na Simba kwa nyakati tofauti.

Advertisement