Mastraika wawili Yanga wasepa

Muktasari:

Wakati Kalengo akiondoka, Issa Bigirimana ambaye inawezekana akawa ameitumikia Yanga katika dakika zisizozidi tano katika ligi naye ameondoka nchini akirejea kwao.

YANGA inajipanga itaingia vipi katika dirisha dogo la usajili lakini wakati kocha wa muda wa kikosi hicho Charles Mkwasa akitaka kuongezewa mastraika wawili, kuna vifaa viwili vimeondoka nchini na kurejea kwao.

Straika wa kwanza kuondoka Yanga ni Maybin Kalengo ambaye baada ya kufanyiwa upasuaji uliokwenda vizuri katika jeraha la kifundo cha mguu ametimka na kurejea kwao Zambia.

Kalengo ameondoka nchini baada ya kuomba ruhusa ya kwenda kujiuguza jeraha lake baada ya kufanyiwa upasuaji uliofanyika hospitali ya Taifa Muhimbili wiki chache zilizopita.

Kalengo ambaye yuko Yanga kwa mkopo wa mwaka mmoja akitokea Zesco ya Zambia, majeraha yake yamekuja wakati mbaya akiwa hajafunga bao lolote huku akishindwa kuanza mechi nyingi katika miezi mitano tangu asajiliwe.

Wakati Kalengo akiondoka, Issa Bigirimana ambaye inawezekana akawa ameitumikia Yanga katika dakika zisizozidi tano katika ligi naye ameondoka nchini akirejea kwao.

Bigirimana ambaye alibeba matumaini ya mashabiki wa Yanga ametumia muda mwingi kuwa majeruhi tangu asajiliwe akicheza mechi moja pekee dhidi ya Ndanda akiingizwa katika muda wa nyongeza akipewa nafasi ya Boniface Mkwasa wakati Yanga ikishinda 1-0 dhidi ya Ndanda ya Mtwara.

Tayari Mkwasa amewasilisha ripoti yake akitaka kusajiliwa mastraika wawili huku washambuliaji hao wakiweka wasiwasi katika kuendelea na klabu hiyo ingawa kuondoka kwake kuna baraka za uongozi.

Mkuchika akubali

Juzi wakati Yanga ikiichapa Coastal Union mabao 3-1 katika mchezo wa kirafiki, Mwenyekiti wa Baraza la Wadhamini la klabu hiyo kapteni George Mkuchika alikuwa jukwaani akifuatilia mchezo huo kisha akasema kidogo anaona mambo yanabadilika.

Mkuchika alisema katika kipindi cha pili ambacho timu yao ilitengeneza mabao hayo ya ushindi aliridhika na soka safi la kutafuta ushindi kwa kushambulia kwa nguvu.

“Nimeridhika na kiwango kuna mambo yanabadilika hasa kipindi cha pili nimeona jinsi vijana wanavyobadilika wanakuja vizuri nafikiri kuna kazi nzuri inafanyika,” alisema Mkuchika.

Aidha, Mkuchika alisema hana matatizo na uteuzi wa Mkwasa kushika majukumu hayo ya ukocha kwa muda kwani eneo hilo ndio taaluma yake halisi anaijua vyema.

“Mkwasa nampongeza kuchukua majukumu haya baada ya uongozi kumuona anafaa. Hili ndio eneo lake ambalo analitumikia kwa taaluma yake na kama unavyoona vijana wanabadilika wanacheza soka la kushambulia,” alisema.