Zahera aweweseka kuwakosa Molinga, Kalengo, Urikhob mechi Pyramids

Muktasari:

Yanga itawakosa washambuliaji wake watatu David Molinga hatocheza mechi hiyo kutokana na kanuni za CAF, Maybin Kalengo aliumia mguu wakati wa mechi ya kirafiki dhidi ya Pamba na Sadney Urikhob aliyeumia wakati wa mchezo uliopita dhidi ya Mbao

Mwanza. Kocha Mkuu Mwinyi Zahera amesema kuwakosekana kwa wachezaji wake watatu inampa wasiwasi kuelekea katika mchezo wake dhidi ya Pyramids utakaochezwa Jumapili kwenye Uwanja wa Kirumba, Mwanza.

Yanga itawakosa washambuliaji wake watatu David Molinga hatocheza mechi hiyo kutokana na kanuni za CAF, Maybin Kalengo aliumia mguu wakati wa mechi ya kirafiki dhidi ya Pamba na Sadney Urikhob aliyeumia wakati wa mchezo uliopita dhidi ya Mbao.

Zahera alisema kuumia kwa Kalengo ni pigo kubwa kwake kuelekea katika mchezo huo.

"Ni kweli wasiwasi upo kwa sababu ni wachezaji waliokuwa na faida kubwa kutokana na walichokifanya, lakini Kalengo alikuwa amekuja vizuri."

Kocha huyo aliongeza kuwa wameamua kufanya mazoezi ya nguvu kutokana na timu wanayoenda kukutana nayo na kwamba anaamini watafunga mabao.

Zahera alisema suala la washambuliaji wake kutotumia vyema nafasi wanazopata anaendelea kulifanyia kazi na kwamba hata mechi ya Jumapili watapata nafasi na watafunga si chini ya mabao mawili.

"Tunaenda kukutana na timu kubwa inayohitaji matokeo mazuri ili kufuzu makundi kama sisi, kwahiyo zile nafasi tulizokosa mechi zilizopita hazitajirudia na ninaamini tutashinda mechi hiyo" alisema kocha Zahera.