Mashabiki Liverpool waipa likizo Corona kisa ubingwa

Muktasari:
- Liverpool imetwaa taji la kwanza la Ligi Kuu ya England baada ya kusubiri kwa miaka 30 tangu ilipolitwaa kwa mara ya mwisho msimu wa 1989/1990
Liverpool,England. Umati wa mashabiki wa Liverpool jana ulilazimika kuvunja masharti na miongozo ya kujikinga na Virusi vya Corona kwa kuamua kuingia mitaani katika maeneo tofauti ya Uingereza ili kusherehekea ubingwa wa Ligi Kuu ya England msimu huu ambao timu yao imeupata jana
Baada ya kusubiri kwa miaka 30, Liverpool jana walitawazwa rasmi kuwa mabingwa kufuatia kipigo cha mabao 2-1 ambacho Manchester City walikipata kutoka kwa Chelsea katika mechi iliyochezwa usiku kwenye Uwanja wa Stamford Bridge jijini London.
Licha ya kuwepo kwa katazo la mikusanyiko ili kukabiliana na kusambaa kwa virusi vya Corona, kwa siku ya jana mashabiki wa Liverpool waliamua kwenda kinyume na katazo hilo na kuamua kuburudika kutokana na furaha waliyokuwa nayo kwa ubingwa huo.
Kutimizwa kwa kiu ya mashabiki hao ya kutwaa taji la kwanza baada ya kusubiri kwa miaka 30 tangu walipotwaa kwa mara ya mwisho msimu wa 1989/1990, kulionekana kuwasahaulisha mashabiki hao na kukiuka masharti na miongozo ya kujikinga na virusi vya Corona ambayo imewekwa na serikali ya Uingereza.
Utamu zaidi wa ubingwa huo ulikuwa kwenye Dimba la Liverpool, Anfield ambako mashabiki walikusanyika na kuanza kusheherekea ubingwa huo kwa kupiga baruti zilizofanya anga zima la Jiji la Liverpool kuwa na rangi nyekundu.
Wachezaji wa Liver nao walionekana kushangilia kwa nguvu ubingwa huo wakiwa wameketi pamoja wanaifuatilia mechi hiyo kwenye runinga na baada ya filimbi ya mwisho kupulizwa walinyanyuka kwenye viti na kuanza kurukaruka huku wakipongezana.
Baada ya mchezo huo uliowapa ubingwa kumalizika kocha mkuu wa Liverpool Jurgen Klopp alifanya mahojiano na kituo cha Skysports na kuelezea furaha yake
" Ni tukio kubwa sana kwangu, sina neno la kuelezea ukubwa huo, siwezi kuelezea juu ya ukubwa wake, sikutegemea kama nitajisikia hivi," aliongea Klopp ambaye alioneokana kushindwa kuyazuia machozi ya furaha.
Kipigo cha mabao 2-1 ambacho Manchester City walikipata kutoka kwa Chelsea kwa mabao ya Christian Pulisic na Willian, kilimaanisha kuwa Liverpool wanakuwa mabingwa rasmi wa Ligi Kuu ya England msimu huu kwai hakuna timu nyingine inayoweza kuzifikia pointi zao 86 hazitoweza kufikiwa na timu nyingine yoyote.
Bao pekee la Manchester City katika mchezo wa jana lilipachikwa na Kevin De Bruyne.